Wednesday, September 20, 2017

Waziri Mkuu atua mkoani Pwani, aacha maagizo mawili Tanzania ya viwanda

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutembelea Mkoa wa Pwani kisha akatoa maagizo mawili kwa uongozi na wananchi kuhusiana na mpango wa Serikali wa kujenga Tanzania ya viwanda.

Katika agizo la kwanza, Majaliwa amewataka viongozi kuboresha miundombinu ya maeneo waliyoyatenga kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ili waweze kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani.

Alisema kuwa ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa viwanda mkoani humo na kuagiza wahakikishe maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji yanakuwa na maji, umeme na barabara.

Kisha, Waziri Mkuu aliwageukia wananchi waliopata ajira katika viwanda viwili alivyovitembelea akiwataka wawe mabalozi wazuri wa Taifa kwa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kuwathibitishia wawekezaji kwamba wana uwezo mkubwa wa kazi na hakuna haja ya kutafuta wafanyakazi kutoka nje ya nchi.

Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza sabuni ya unga cha Keds kilichopo Kibaha na kile cha vigae cha Twyford kilichopo Chalinze.

Alisema mbali na viwanda hivyo kutoa ajira nyingi kwa Watanzania, pia vitakapoanza uzalishaji vitawawezesha wananchi kupata bidhaa mbalimbali kama vigae kwa bei nafuu kwa kuwa vitakuwa vinazalishwa nchini.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa viwanda hivyo, Jack Feng alisema ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 90 na sasa wako katika hatua za mwisho ikiwa ni pamoja na ufungaji mitambo na vinatarajiwa kuanza uzalishaji Oktoba.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alimuomba waziri mkuu asaidie upatikanaji wa nishati ya umeme ya kutosha kuweza kuendesha viwanda katika mkoa huo.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )