Sunday, October 29, 2017

JWTZ kukarabati madaraja yaliyosombwa na mvua Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema serikali inaendelea na jitihada za kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa na mvua, zilizonyesha hivi karibuni ili wananchi waendelee na shughuli za kiuchumi.

Aidha, Makonda amesema Benki ya Dunia imetoa Sh bilioni moja kwa ajili ya kusafisha eneo la Jangwani, bonde la Mto Msimbazi na kazi ya usafishaji inatarajiwa kuanza wiki ijayo baada ya kukamilisha hatua za kumpata mkandarasi.

Makonda alisema hayo jana wakati wa ziara ya kukagua athari, zilizosababishwa na mvua hizo katika maeneo mbalimbali ya jiji na kuliagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujenga daraja la muda katika eneo la Mbezi Beach Daraja la Malecela, lililoharibika kutokana na mvua hizo.

“Wakati Tanroads wanaendelea kurejesha miundombinu katika hali ya kawaida, Jeshi letu la (JWTZ) litatusaidia kujenga daraja la muda ili kuhakikisha watu wanapita na kuendelea na shughuli zao, niwaombe tu muwape ushirikiano wakati wakifanya kazi hiyo na mimi naamini watafanya haraka na itapitika muda mchache,” alisema wakati akiongea na wananchi wa maeneo hayo.

Aidha, Makonda alisema mbali na barabara na madaraja, pia wahusika wa umeme na maji, wanaendelea na jitihada ili kuhakikisha miundombinu hiyo inarejea na wananchi kuendelea kupata huduma hizo muhimu.

Hata hivyo, Makonda aliwataka watu wanaoishi katika maeneo hatarishi, kuondoka katika maeneo hayo ili kujiepusha na hatari wanazoweza kuzipata, kwa kuwa mvua hizo bado zinaendelea kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).

Pia Makonda aliwataka wananchi wenye tabia za kuchimba michanga kwenye mito, kuacha kwa kuwa kitendo hicho kwani kinachangia uharibifu mazingira, ambayo yanawaadhibu sasa.

“Serikali inapotoa rai, siyo kwamba inawachukia inawatakia mema, niwaombe tena leo kwa unyenyekevu tuchukue tahadhari, ni kwa faida yako na familia yako, kuna baadhi tumeziba mito wengine wamefanya dampo na wengine kuchimba mchanga, jambo ambalo linaongeza madhara kuwa makubwa, ningeomba tu muwe mnatii tahadhari zinazotolewa na serikali,” alisema Makonda.

Alisema kwa Manispaa ya Kinondoni pekee, kuna nyumba 200 ambazo zipo kwenye maeneo hatarishi huku nyumba 190 zikiwa zimebomoka, hivyo ni vyema wananchi hao wakaendelea kuchukua tahadhari ili kuepusha madhara zaidi.

Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )