Tuesday, October 3, 2017

Katibu mkuu Wizara ya viwanda na biashara astaafu

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia maendeleo ya viwanda, Dk Adelhelm Meru amestaafu utumishi wa umma huku akiwataka watumishi wa wizara hiyo wasameheane.

“Kwa kipindi tulichokuwa pamoja kuna mengi tuliyakamilisha. Naomba tusameheane tulipokosana kwa sababu hakuna mkamilifu,” alisema Dk Meru ambaye anatarajia kujielekeza kwenye ujasiriamali muda mfupi ujao.

Dk Meru aliteuliwa na Rais John Magufuli kushika nafasi hiyo Desemba 2015 kabla hajastaafu wiki iliyopita kuhitimisha miaka 37 ya utumishi wake.

Licha ya wizara hiyo yenye makatibu wakuu wawili ambayo sasa itabakiwa na mmoja, Wizara ya Nishati na Madini imebakiwa na naibu baada ya aliyekuwa katibu mkuu wake, Profesa Justin Ntalikwa kutumbuliwa mwishoni mwa Machi na nafasi yake kubaki wazi mpaka sasa.

Akizungumza kwenye hafla ya kumuaga, Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage alimpongeza kwa kumaliza salama utumishi wa umma na kumsifu kwa umahiri wake katika kutekeleza sera ya maendeleo ya viwanda. “Ulikuwa mstari wa mbele kubuni mbinu na mikakati ya kuharakisha ujenzi wa viwanda nchini,” alisema Mwijage.

Dk Meru aliwashukuru wafanyakazi wa wizara hiyo kwa ushirikiano waliompa na kuwaomba waendelee nao kwa watendaji wengine katika kuijenga Tanzania ya viwanda.

Kustaafu kwa Dk Meru ambaye alikuwa mkurugenzi mkuu wa kwanza Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) kunaongeza nafasi za watendaji ambao Rais Magufuli anapaswa kuzijaza. Nafasi nyingine zilizo wazi kwa sasa ni ile ya waziri na katibu mkuu wa nishati na madini.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )