Tuesday, October 3, 2017

Mwenge wamtia matatani mkurugenzi wa halmashauri Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella amempa siku mbili Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Kazimbaya Makwega kuhakikisha anawasilisha taarifa ya ujenzi wa darasa la Shule ya Msingi Mkundiambaru.

Hatua hiyo inatokana na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kukataa kulizindua baada ya kubainika limejengwa chini ya kiwango.
 
Agizo hilo amelitoa leo Jumanne katika Uwanja wa Ndege wa Tanga baada ya kiongozi huyo wa mbio za Mwenge, Amour Hamad Amour kueleza akiwa wilayani Lushoto Septemba 22 aligoma kuzindua darasa hilo kutokana na kuwepo dosari kuu tatu.
 
Akizungumza wakati akiwaaga viongozi wa Mkoa wa Tanga kuelekea Kusini Pemba leo, Amour amezitaja dosari hizo kuwa ni darasa dogo lisilokidhi vigezo, lina nyufa na limeezekwa kwa mabati ya geji 32 badala ya 28 zinazotakiwa kwenye majengo ya Serikali.
 
“Tukiwa Lushoto nilimwagiza kabla ya kuondoka Tanga leo awe ameniletea Bill of Quantities –BOQ (mchanganuo wa makadirio ya kazi) na hati ya ununuzi wa vifaa vya mradi lakini nasikitika kuwa hajaleta. Kwa hiyo, nampa siku nne awe ametuletea Pemba ili tuweze kupeleka taarifa kwa viongozi wetu,” amesema Amour.
 
Darasa hilo lilipangwa kuzinduliwa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Lushoto.
 
Makwega katika taarifa baada ya Amour kugoma kulizidua jengo hilo alieleza  lilijengwa kwa nguvu za wananchi waliotumia Sh7 milioni badala ya Sh11 milioni zilizohitajika.
 
Kuhusu mabati alisema yameezekwa ya muda na kwamba, uongozi wa halmashauri umepanga kuyaondoa na kuezeka mengine.

Majibu hayo hayakumridhisha Amour aliyemuagiza kuwasilisha BOQ na hati ya ununuzi wa vifaa vya mradi huo kabla Mwenge haujakabidhiwa Kisiwani Pemba.
 
“Hadi leo tumepita mikoa 26, mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ndiye aliyetukwaza, tulimwagiza kabla hatujatoka Tanga awe ameleta taarifa ya darasa hilo lakini hadi sasa Oktoba 3 hatujamuona. Tunakuomba RC mweleze kuwa awe ameleta ndani ya siku nne tutakazokuwa Pemba,” amesema Amour.
 
Mkuu wa mkoa, Shigella amesema atahakikisha taarifa hiyo inawasilishwa kwa kiongozi huyo kesho Jumatano.
 
“Wewe umetoa siku nne, mimi namwagiza kesho awe ameshawasilisha taarifa hiyo,” amesema Shigella.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )