Thursday, November 2, 2017

NEC yavionya vyama vya siasa katika uchaguzi mdogo

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani amevitaka vyama vya siasa na wagombea wanaoshiriki uchaguzi mdogo wa madiwani kutekeleza na kuheshimu maadili ya Uchaguzi na kuonya kuwa chama au mgombea atakayekiuka maadili hayo atachukuliwa hatua kama ilivyoanishwa chini ya Kifungu cha 124A cha Sheria ya Uchaguzi Na.1 ya mwaka 1985.

Akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya Uchaguzi huo Madiwani utakaofanyika Novemba 26 mwaka huu amevitaka vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinawaelemisha wafuasi wao juu ya kutekeleza maadili hayo katika kipindi chote cha kampeni.

Amesema iwapo wafuasi wa vyama vya siasa watavunja maadili hayo, chama husika pamoja na mgombea wake kitachukuliwa hatua za kinidhamu.

Mkurugenzi Kailima amevitaja vitendo vinavyokiuka maadili ya uchaguzi kuwa ni pamoja na wagombea au wafuasi wa vyama hivyo kuchana mabango ya wagombea wengine, kutoa lugha chafu wakati wa mikutano ya kampeni pamoja na kupitisha muda wa kufanya mikutano ya kampeni.

Amezitaka kamati za maadili za kata na jimbo kuchukua hatua kali kwa chama au mgombea ambaye atavunja maadili hayo. Amesema kamati hizo zinatakiwa kuchukua hatua ndani ya saa 48 mara chama au mgombea anapovunja maadili.

Amesema kuwa miongoni mwa adhabu zinazowakabili wagombea au chama ambacho kitakiuka maadili ya uchaguzi ni kuomba radhi wananchi hadharani, kutotumia vyombo vyha habari kwa muda fulani, onyo la maandishi kusimamishwa kufanya kampeni, mgombea kutangaza mbele ya vyombo vya habari kuwa yeye ni bingwa wa kuvunja maadili ya uchaguzi au kutozwa faini Sh 100,000.

Kailima pia amesema chama cha siasa ambacho kinataka kufanya mabadiliko ya ratiba ya mikutano ya kampeni, lazima kimfahamishe msimamizi wa uchaguzi wa kata na ombi hilo lazima lijadiliwe na vyama vyote vinavyoshiriki kwenye uchaguzi.

Kuhusu vitambulisho mbadala vitakavyotumika wakati kupigia kura kwa wale ambao wamepoteza kadi ya mpiga kura ambavyo ni vitambulisho vya taifa, leseni ya udereva na hati ya kusafirisha; Kailima amesema vitambulisho hivyho vitatumika tu kwa watu ambao wameandikishwa katika kituo husika mwaka 2015, lakini pia bado wana sifa za kupiga kura.

Amesema vitambulisho hivyo vitatu hata kama vimeisha muda wake, mhusika anaruhusiwa kupiga kura. “Pale tunachoangalia ni uthibitisho wa mtu sio kwamba anasafiri au anaendesha gari, pia tunaamini kuwa vimetolewa na mamlaka husika.

Kailima ametoa mwito kwa vyama vya siasa kutambua kwamba tume ya taifa ya uchaguzi imeruhusu mikutano ya kampeni na sio mikutano ya vyama vya siasa. Amesema mtu anayeruhusiwa kwenye mikutano ya kampeni ni mgombea mwenyewe, chama chake au mtu yeyote ambaye anaona anaweza kumfanyia kampeni ndani ya katiba iliyopitishwa.

Amesema tume imepokea rufaa 14 kutoka kwa wagombea ambao hawakuridhika na maamuzi yaliyotolewa na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo. Amesema wataanza kusikiliza rufaa hizo Ijumaa na Jumatatu ijayo watakuwa wameshatoa uamuzi.

Wakati huo huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26, 2017 katika kata 43 utagharimu kiasi cha Sh bilioni 2.5.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Ramadhani Kailima, amesema msingi wa bajeti ya uchaguzi unategemea idadi ya vituo vya kupigia kura na idadi ya wapiga kura waliokuwepo katika kata husika. Amesema idadi ya watu ndio inatoa bajeti ya karatasi za kupigia kura pamoja na vituo ambavyo vinakuwa na watumishi wasiopungua wanne.

Amesema katika kituo cha kupigia kura kina watumishi msimamizi wa kituo, msaididzi, karani mwongozaji na mlinzi wa kituo “lakini pia kuna watu wa ziada wako ngazi ya kata na jimbo ambao wanaweza kutumika iwapo msimamizi wa kituo na msaidizi wake wameapata dharura.

Kailima amesema kwamba kata yenye vituo 40 ina bajeti kubwa kuliko kata yenye vituo vichache. Amesema bajeti hiyo pia inategemea askari wanaosimamia uchaguzi na umbali ambako uchaguzi huo unafanyika.

Amefafanua kuwa gharama zingine za uchaguzi ziko kwenye usafirishaji wa vifaa kwenda kwenye kata ambako uchaguzi unafanyika pamoja na machapisho mbalimbali yatakayotumika kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )