Friday, November 24, 2017

Rais Magufuli atuma salamu za rambirambi kifo cha Mbunge wa Songea Mjini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Mhe. Leonidas Tutubert Gama.

Mhe. Leonidas Tutubert Gama amefariki dunia jana tarehe 23 Novemba, 2017 saa 4:25 usiku katika hospitali ya Mtakatifu Joseph ya Peramiho, iliyopo Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma ambako alikimbizwa kwa matibabu baada ya kuugua ghafla.

“Nimepokea kwa mshtuko na majonzi taarifa za kifo cha ghafla cha Mhe. Leonidas Tutubert Gama, nakupa pole Mhe. Spika Job Ndugai, Wabunge na wafanyakazi wa ofisi yako, na kupitia kwako naomba ufikishe salamu zangu za pole kwa familia ya Marehemu, wananchi wa Jimbo la Songea Mjini na Mkoa mzima wa Ruvuma, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempa pole Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma Ndg. Oddo Mwisho na wana CCM wote kwa kumpoteza kada wao aliyeiwakilisha vizuri CCM kwa nafasi yake ya ubunge.

Mhe. Rais Magufuli amesema Mhe. Leonidas Tutubert Gama ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa na Mbunge, alikuwa kiongozi hodari, aliyefanya kazi kwa kujiamini na aliyependa kupigania maslahi ya wananchi bila kuchoka.

Amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi na pia ameiombea familia yake iwe na subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.

Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe, Amina.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Novemba, 2017
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )