Tuesday, November 14, 2017

Viongozi taasisi ya mikopo elimu ya juu ( TSSF) watiwa mbaroni

Viongozi wa  Taasisi ya Kusaidia Jamii ( TSSF) ambayo ilitangaza kuwa inatoa mikopo ya elimu ya juu wamekamatwa na polisi baada ya kugundulika kuwa ni matapeli.

Wakurugenzi hao wamekamatwa jana Jumatatu jioni mara tu baada ya mkutano wa waandishi wa habari na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha wa kuelezea kuhusu uchunguzi uliofanyika baada ya Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi kuomba mwongozo bungeni.

Chumi alitaka ufafanuzi kuhusu uhalali wa taasisi hiyo baada ya kutangaza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kulipa Sh 30 000 kama ada ya maombi ya kusajiliwa kuomba mkopo.

Hata hivyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema  Serikali haitambui taasisi hiyo na kuahidi kufanya uchunguzi.

Akizungumza leo Jumanne, Ole Nasha amesema baada ya uchunguzi huo wamebaini kuwa taasisi hiyo haina uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 50,000 ambao ilitangaza kutoa.

Amesema katika mahojiano na taasisi hiyo viongozi hao walisema kuwa fedha za kuwakopesha wanafunzi hao watazipata kutoka nje ya nchi baada ya kupeleka kiasi cha fedha.

Hata hivyo, amesema mkataba wa taasisi hiyo na wafadhili hao unaonyesha kuwa wamefikia makubaliano ya kufanya utafiti wa jinsi wanavyoweza kukusanya fedha na si kuwapa fedha kwa ajili ya kutoa mikopo.

Amesema tayari taasisi hiyo imekusanya fedha kwa wanafunzi 600 na imepeleka wanafunzi 198 katika vyuo mbalimbali nchini kwa makubaliano ada zao wangelipa Desemba mwaka huu.

Hata hivyo, amesema hakuna uthibitisho kama wana fedha kweli za kuwalipia wanafunzi hao ada ingawa wanadai kuwa katika akaunti zao za benki wana fedha kati ya Sh 600 milioni na 700 milioni.

Amesema kufuatia hilo wanaagiza vyombo vya dola kuchunguza jambo hilo na wakati wakifanya hivyo ni marufuku kwa vyuo kuwapokea wanafunzi wanaopewa mikopo na taasisi hiyo.

Pia ameagiza akaunti zao zote kufungiwa hadi hapo watakapomaliza uchunguzi sambamba na taasisi hiyo kutojihusisha na shughuli yoyote.

Baada ya kumaliza mkutano huo polisi kutoka makao makuu ya polisi waliingia ndani ya ukumbi wa mkutano na kuwaeleza wako chini ya ulinzi.

Polisi hao mmoja akiwa na sare na mwingine akiwa na nguo za kiraia waliwakamata na kuondoka nao.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )