Thursday, November 30, 2017

Wabunge CHADEMA Wanyimwa Dhamana na Kupelekwa Mahabusu

 Wabunge wawili wa Mkoa wa Morogoro kupitia Chadema pamoja na washtakia wengine 34 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro kujibu mashtaka nane yanayowakabili likiwemo la kuchoma moto ofisi ya Kata ya Sofi iliyopo wilayani Malinyi.

Wabunge hao ni Susan Kiwanga(Mlimba) na Peter Lijualikali(Kilombero) na baada ya kusomewa mashataka hayo upande wa mashtaka uliwasilisha mahakamani hapo hati ya kiapo cha kupinga dhamana yao kwa madai kuwa wataharibu upelelezi wa kesi hiyo.

Kesi hiyo ya jinai namba 296 iliyovuta hisia za wakazi wengi wa manispaa ya Morogoro ilisomwa mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Ivan Msack ambapo upande wa mashtaka ulikuwa ukiongozwa na wakili wa Serikali, Edga Bantulaki na Sunday Hyera huku washtakiwa hao wakitetewa na wakili Bartalomew Tarimo.

Akisoma mashtaka hayo leo Alhamisi huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa ndani na nje ya mahakama Wakili Bantulaki alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda makosa hayo Novemba 26 mwaka huu katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi.

Alidai kuwa bila uhalali huku wakijua kufanya hivyo ni kosa washtakiwa hao walikula njama na kuchoma moto ofisi ya kata hiyo sambamba na kufanya uharibifu wa mali mbalimbali za ofisi hiyo.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa wote walikana kuhusika na hivyo mahakama kuaihisha kesi hiyo hadi Desemba 5 mwaka huu kwa ajili ya kutolewa maamuzi ya dhamana.

Kabla ya kufikishwa mahakamani hapo Lijualikali alijisalimisha katika kituo cha polisi Morogoro majira ya saa nne asubuhi baada ya jeshi la polisi kutangaza kumtafuta.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )