Monday, December 4, 2017

BomoaBomoa Ilivyoacha Kilio na Majonzi Dodoma

Vilio vimetawala katika  bomoabomoa kwa watu waliojenga katika eneo la hifadhi ya kampuni ya Miliki ya Raslimali za Reli (Rahco) ambapo jumla ya nyumba 128 na vibanda vidogo 487 vimebomolewa katika eneo hilo.

Watu hao waliwekewa alama za X  wakitakiwa kubomoa  kwa hiari yao Novemba 25 mwaka jana kwa mara ya mwisho wakitakiwa kupisha eneo la hifadhi ya reli walilovamia.

Akizungumza jana Desemba 3  mara baada ya kukamilisha zoezi hilo, Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Catherine Moshi alisema bomoabomoa hiyo ilihusisha vibanda vya stendi ya daladala ya Jamatini, vibanda vya stendi ya mabasi ya kwenda mikoani, Ofisi za kampuni ya mabasi ya Shabiby na Abc, Mgahawa wa Cape Town na kituo kimoja cha mafuta kilichokuwa karibu na ofisi za Shabiby.

Kuhusu stendi ya mabasi, amesema wamekubaliana na uongozi wa mkoa na manispaa kuwapa muda wa kuondoa stendi mbili za mabasi yaendayo mkoani na ya daladala ya Jamatini.

“Wamesema kuondoa stendi sasa italeta shida kwa hiyo kuna makubaliano ambayo tumekubaliana na Mkuu wa Mkoa (Dk Binilith Mahenge) wa kutoa muda wa wao kuzihamisha,”alisema.

Hata hivyo, alisema makubaliano yao si kwamba stendi hizo zinabaki bila kubomolewa bali ni kwa muda na ukiisha wawe wamepata eneo la kupeleka huduma hizo ili eneo libaki tupu likabidhiwe kwa mkandarasi.

Alisema wamemaliza kazi hiyo kwa Dodoma mjini isipokuwa maeneo ya kanisa, misikiti, makaburi na ambayo mahakama imezuia ikiwemo kituo cha mafuta kilichomo mkabala na stendi ya daladala ya Jamatini.

Moshi  amesema  wamebomoa nyumba kamili 128 na  vibanda 487 ambazo waliziwekea alama lakini wapo wengine walioamua kujiondoa wenyewe.

Amesema kuwa walishasaini mkataba na mkandarasi Novemba 29 mwaka huu  na kwamba kabla ya kumkabidhi mkandarasi eneo hilo ni lazima wahakikishe kuwa njia ya reli ziwe safi.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, John Banda alisema kuwa makubaliano na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge yaliyofanyika Ijumaa hayakutekelezwa baada ya kufika katika eneo hilo Jumamosi akiwataka wafanyabiashara hao kuondoka.

Awali wafanyabiashara hao waliomba kupewa muda wa kuhama na kuonyesha eneo jingine la kufanyia biashara baada ya kuondolewa katika eneo hilo.

“Jumamosi Mkuu wa mkoa alifika katika eneo hilo kuwapelekea wafanyabiashara majibu aliyoyapata baada ya kukutana na kamati yake ya ulinzi na usalama. Aliwaambia watu wa Jamatini ni vyema kila mmoja aondoe kibanda chake yeye mwenyewe,” amesema.

Amesema kuwa amekwenda kule (kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa) amepata elimu. Amekuja kuwaletea majibu ya kamati ya ulinzi na usalama kuwa ni vizuri kubomoa wenyewe kabla ya kusubiri kuondolewa.

Amesema kuwa eneo walilopelekwa la Makole lilopo nyuma ya mahakama halina biashara kwa sababu wateja wao wakuu walikuwa wakiwategemea ni abiria wanaotumia stendi hizo.

“Eneo hilo (Makole) lina vumbi sawa lina miundombinu ya vyoo na nini. Lakini kikubwa kule hakuna biashara kwa sababu wateja wetu ni abiria,” amesema.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )