Friday, December 29, 2017

Kiwanda cha Alizeti Mount Meru Millers Ltd kimefungiwa

Serikali imekifungia Kiwanda cha kukamua mafuta cha  Alizeti Mount  Meru Millers Ltd   muda usiojulikana kwa madai ya kukaidi agizo la kulipa faini ya Sh20milioni.

Uamuzi wa kukifunga kiwanda hicho umetolewa  Jumatano na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira ,Kangi Lugola  alipokuwa kwenye kwanda hicho kilichopo  kijiji cha Manguanjuki Manispaa ya Singida.

Kabla ya kutoa uamuzi huo  mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Singida, Lugola alisema Novemba 29 mwaka jana, mtangulizi wake Luhaga  Mpina, aliuagiza uongozi wa  kiwanda hicho ulipe  faini ya Sh20milioni kwa kosa la kutiririsha  maji taka yenye kemikali kwenye makazi ya watu .

“Maji taka yameelekezwa kwenye makazi ya wananchi wanaokizunguka kiwanda .Pia maji  hayo yenye kemikali, yameelekezwa kwenye ziwa la Singidani lenye viumbe hai wakiwemo samaki. lakini hadi leo, agizo la Waziri  Mpina, halijatekelezwa’’ amesema Lugola na kuongeza kwamba

‘’Kutokana na  ukiukwaji wa  sheria za mazingira, Mpina alikipa adhabu ya kulipa faini  Sh20milioni ambayo haijalipwa hadi leo”, amesema Waziri Lugola kwa masikitiko.

Lugola amesema kwamba  kiwanda hicho kimetekeleza agizo la kununua mashine ya kutibu maji taka, lakini maji taka hayo, hayajaelekezwa kwenye mashine hiyo.

 “Maji hayo yenye kemikali bado yameendelea kuwa kero kwa wananchi hadi leo, na yanaathiri viumbe hai vilivyopo kwenye ziwa Singidani. Hii dharau kwa serikali haikubaliki”, amesema

Naibu waziri huyo, amesema  wananchi wanaozunguka kiwanda hicho wamekuwa wakitoa kilio chao serikalini kwa miaka minne, kwamba wanaathiriwa na maji yenye kemikali  na moshi mnene wa kiwanda cha Maount Meru.

“Binafsi leo nimefika kwenye kiwanda hiki na baada ya kufanya ukaguzi wa kina, nakiri kwamba kilio cha wananchi wa Manguanjuki ni cha kweli na kinahitaji tiba ya kudumu. Mkuu wa wilaya ya Singida, naagiza kuanzia sasa, usimamie kufungwa kwa kiwanda hiki”,amesema na kuongeza;

“OCD pia nakuagiza uwatafute Wakurugenzi wa kiwanda hiki Atul Nittal, Arvind Mittal na Tarsem Aggarwal, popote walipo na kuwakamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria kwa kukaidi agizo la Serikali”.

Kwa upande wake meneja Uhusiano, Nelson Mwakambuta, amesema kiwanda hicho kimekuwa kikifanyiwa ukaguzi mara kwa mara na mamlaka mbalimbali. Lakini  wamekuwa wakiaambiwa na viongozi hao kuwa   kiwanda hicho, hakina tatizo lolote linalohusiana na kwenda kinyume na sheria za  mazingira.

“Kufungwa kwa muda usiojulikana kwa kiwanda hiki, kutaathiri ustawi wa watumishi wengi wa kiwanda na familia zao. Pia  wakulima wa zao la alizeti ndani na nje ya mkoa wa Singida, nao watakuwa wamepata pigo. Hatupingani na serikali tutatekeleza yale yote tuliyoagizwa”,amesema meneja huyo.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )