Monday, December 4, 2017

Mchungaji Rwakatare aomba Rais Magufuli aungwe mkono

Askofu wa Kanisa la Assemblies of God maarufu Mlima wa Moto, Dk Getrude Rwakatare ametoa wito kwa wananchi kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kusimamia rasilimali za Taifa.

Akihubiri katika kongamano la Shiloh lililotumika kuliombea Taifa amani jana Jumapili Desemba 3,2017, Mchungaji Rwakatare alisema katika miaka miwili aliyokaa madarakani, Rais Magufuli  amefanya mambo mengi katika kusimamia rasilimali za nchi, kupambana na rushwa, ubadhirifu na kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma.

“Ili kumuunga mkono Magufuli ni lazima kila Mtanzania atimize wajibu wake katika kujiletea maendeleo yake na ya Taifa kwa jumla,” alisema katika kanisa lake lililopo Mikocheni B wilayani Kinondoni.

Mchungaji Rwakatare alisema wananchi wanaolalamika kwamba hali ya maisha ni ngumu ni lazima wabadilike na kuacha kuishi maisha ya kuigiza.

“Tuvae viatu vinavyotutosha kwa kuishi maisha yanayolingana na kipato chetu, tusiishi maisha ya kuigiza mambo ambayo hatuna uwezo nayo,” alisema.

Mchungaji Rwakatare alisema wananchi wanatakiwa kubadilika kwa kuwa fedha za ujanjaujanja ni vigumu kuzipata kutokana na Serikali kuziba mianya ya ubadhirifu.

Kuhusu kongamano hilo, alisema hufanyika kila mwaka likilenga kumshukuru Mungu kwa mambo ambayo amewafanyia.

“Tunapomaliza mwaka ni lazima tumshukuru Mungu kwa mambo ambayo ametufanyia na kuliombea Taifa kwa ajili ya mwaka 2018,” alisema.

Kabla ya maombi, waumini wa kanisa hilo waliimba wimbo wa Taifa wakiwa wameshika bendera za Taifa.

Mchungaji wa kanisa hilo kutoka Arusha, Dk Dastan Maboya alisema ni muhimu kuwaombea viongozi ili wafanye uamuzi wenye masilahi kwa Taifa.

“Amani iliyopo si kwa sababu imeshuka kutoka mbinguni bali ni misingi bora iliyofanywa na waasisi wa Taifa hili, tuwaombee viongozi waliopo waendelee kufuata nyayo zao,” alisema.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )