Loading...

Thursday, December 7, 2017

Mvutano waibuka kesi ya Madabida na wenzake....Mahakama kutoa uamuzi Kesho

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho Ijumaa inatarajiwa kutoka uamuzi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano  kama ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo ama la.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Utatolewa baada ya kusikilizwa hoja zilizowasilishwa na upande wa mawakili wa Serikali, Pius Hilla na Shedrack Kimaro na mawakili wa utetezi, Denis Msafiri, Makaki Masatu na Nehemia Nkoko.

Wakili wa Serikali, Kimaro akiwasilisha hoja zao leo Alhamisi alidai kuwa hoja ya mawakili wa utetezi kuwa Mahakama ya Kisutu ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo kwa sababu ipo chini ya Sh 1 bilioni siyo sahihi.

Amedai kuwa ni dhahiri kuwa makosa hayo ni ya uhujumu uchumi na mamlaka yenye mamlaka ya kuisikiliza ni Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi.

“Hivyo mahakama za chini kama Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo labda kuwepo na kibali cha kulipa mamlaka ya kuisikiliza kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).”

Kutokana na hilo aliiomba Mahakama kutupilia mbali hoja za upande wa utetezi.

Wakili wa utetezi, Msafiri alidai kuwa ameusikia upande wa mashtaka, ila ni rai yao kuwa marekebisho ya sheria ya uhujumu uchumi ya 2016 yanaipa moja kwa moja Mahakama ya Kisutu kuisikiliza kesi hiyo.

Alidai kuwa kosa lolote lililopo chini ya Sh 1 bilioni haliwezi kusikilizwa na Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi ni Mahakama za chini ikiwamo Mahakama ya Kisutu.

Alisisitiza kuwa Mahakama ya Kisutu ina mamlaka kamili ya kuisikiliza kesi hiyo kwa vile shtaka halizidi Sh 1 bilioni na kwamba mahakama hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo na siyo Mahakama Kuu.

Pia alidai kuwa kibali cha DPP cha kuipa mamlaka mahakama kusikiliza kesi kinapaswa kipelekwe mahakamani pamoja na hati ya mashtaka.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Ijumaa ambapo mahakama itatoa uamuzi na washtakiwa waliamuliwa wapelekwe polisi.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Pius Hilla aliomba wapelekwe magereza kwa sababu washtakiwa hao kuendelea kuwa mikononi mwa polisi kuna suala la gharama na polisi hawana fungu.

Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Wakili Nkoko aliomba Mahakama kusimamia amri yake kama ilivyoitoa.

Wakili Masatu naye aliiomba mahakama iendelee na oda yake ilivyoitoa jana Jumatano.

Hakimu Nongwa amesema suala la gharama hawawezi kulikwepa pale haki inapotafutwa na kuamuru washtakiwa wapelekwe polisi hadi kesho Ijumaa atakapotoa uamuzi kama mahakama hiyo ina mamlaka ama la.

Madabida na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi ikiwamo kusambaza dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi ' ARV’s ' na kusababisha hasara ya Sh 148 milioni.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )