Monday, January 1, 2018

CHADEMA Kuja na Mikakati Mipya 2018....Isome Hapa

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza mikakati ya chama chake kwa mwaka 2018, akisema kitapigania upatikanaji wa Katiba Mpya ikiwemo uwepo wa tume huru ya uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam jana, Mbowe alisema licha ya kutambua kuwa mwaka 2017 ulikuwa mgumu kwa vyama vya upinzani, mwaka huu watahakikisha wanapambana ili kurudisha mchakato wa Katiba mpya.

“Jambo kubwa tunalopigania hapa ni kuwa na tume huru ya uchaguzi,” alisema.

Moja ya mambo yanayolalamikiwa kuwa chombo hicho hakina uhuru ni uteuzi wa viongozi wake kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, na muundo wake.

Kwa sasa, NEC ina wafanyakazi wa ofisi ya makao makuu tu, wakati katika ngazi za wilaya ambako uchaguzi huratibiwa, inategemea wakurugenzi wa halmashauri ambao pia ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa chombo hicho.|

Katika mkutano wa jana, Mbowe alisema suala la ukosefu wa fedha ili kuendelea na mchakato huo halina mashiko kwa kuwa kinachohitajika ni dhamira ya dhati.

“Tumeshatumia fedha nyingi hadi kufikia mchakato wa Katiba mpya ulipoishia, kinachohitajika ni dhamira ya dhati ya kupata Katiba Mpya. Rais anatakiwa kutambua kuwa Katiba ni matakwa ya wananchi si mapenzi ya Rais,” alisema.

Aliwataka wadau kutoviachia vyama vya siasa pekee kudai Katiba mpya kwa kuwa ina manufaa kwa Watanzania wote.

Mbowe alisema watahakikisha wanatumia kila aina ya mbinu ili kufanikisha kuendelea na mchakato huo.

“Leo tunamaliza mwaka 2017 lakini kwetu ulikuwa mgumu kushinda yote tangu nchi iingie katika demokrasia ya vyama vingi miaka 25 iliyopita,” alisema.

Alisema licha ya kuijenga demokrasia kwa kipindi chote hicho, utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano umerudisha nyuma.

“Pamoja na kuwa mimi ni mwenyekiti wa Chadema siwezi kuitisha mkutano wa wanachama hapa Dar es Salaam,” alisema.

Mchakato wa Katiba Mpya ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2011 alipounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Hata hivyo, mchakato huo uliishia kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambalo licha ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ambayo haijapigiwa kura ya maoni hadi leo, baadhi ya vyama vya upinzani vilijitoa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kikiwemo Chadema na kupinga mchakato huo kwa maelezo kuwa ulivurugwa na chama tawala.

Vyama vya upinzani vimejikuta katika wakati mgumu tangu kuingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na kushindwa kufanya mikutano ya hadhara, viongozi wake kukamatwa kwa tuhuma za uchochezi, kufanya fujo na uharibifu.

Mbowe alisema wakati vyama vya upinzani vinakatazwa kufanya mikutano, chama tawala kinafanya.

“Hakuna usawa katika kufanya siasa, ni sawa na kumfunga mikono bondia halafu unataka apigane na mwenzake ambaye hajafungwa mikono,” alisema.

Mbowe alisema kama Serikali inaona hakuna umuhimu wa kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa ni bora vikafutwa kuliko kuvizuia visifanye siasa.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )