Loading...

Tuesday, January 30, 2018

Wanaokopa Matrilioni Nje Ya Nchi Kwa Dhamana ya Ardhi ya Tanzania Kubanwa Zaidi

Bunge  limesema limebaini ardhi ya Tanzania imewekwa dhamana ya mkopo katika benki za ughaibuni na baadhi ya Watanzania na raia wa kigeni waliokopa matrilioni ya shilingi.

Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa

Mchengerwa alisema kamati yake, mbali na mambo mengine, imetaarifiwa na serikali kuwa kuna Watanzania na Wakenya wachache wamekopa matrilioni ya shilingi katika benki za ughaibuni wakiweka dhamana mashamba yaliyopo nchini.

Alisema changamoto hiyo ndiyo iliyoilazimu serikali kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na.5 wa Mwaka 2017 ambao umeigusa Sheria ya Ardhi, ili kutunga sheria ambayo itaondoa mwanya huo, akidokeza kuwa Sheria ya Ardhi iliyopo ina dosari ya kutokuwa na kipengele kinachodhibiti hali hiyo.

Muswada huo unaotarajiwa kusomwa kujadiliwa katika mkutano wa 10 wa Bunge la 11 unaoanza leo, ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni Novemba, mwaka jana, wakati wa mkutano uliopita wa chombo hicho cha kutunga sheria.

Mchengerwa alisema kamati yake ilipata wiki mbili kwa ajili ya uchambuzi wa muswada huo na kubainisha kuwa wameuboresha kwa kiasi kikubwa.

"Kwa historia na taarifa ambazo tumepewa, kuna Watanzania, wale wa juu kidogo ambao wao wamekwenda kukopea mashamba yetu ambayo yako wazi. Wamekwenda kukopa matrilioni ya shilingi nje ya Tanzania wakiweka dhamana mashamba yetu, na mashamba haya yako wazi, hayajaendelezwa," alisema.

Mchengerwa alisema zaidi: "Na tunaamini sheria hii tukiipitisha na kama mikopo itakwenda kuboresha mashamba, naamini Tanzania tutapiga hatua kubwa sana kwa sababu kama leo hii zaidi ya Sh. trilioni moja, trilioni mbili ziko nje ya nchi au zimekopewa na watu katika mashamba makubwa ambayo tunayaona yana miti, hayajaendelezwa kabisa, na aliyekopa alidhamiria kwenda kujenga kiwanda kwenye eneo lilelile au kulima kilimo fulani na hajakiendeleza, inamaanisha zile Sh. trilioni mbili zingeiingia Tanzania na kile kilimo kingelikuwa na tija."

Mbunge huyo wa Rufiji (CCM) alibainisha kuwa muswada huo ulipowafikia ulikuwa unagusa watu wote, lakini wameuboresha kwa kuondoa kipengele kinachozuia hata wananchi wa kawaida kukopa fedha benki kwa kuweka dhamana ya ardhi wanayoimiliki.

Alisema kwa sheria mpya itakayotungwa, madhumuni ya mkopo kwa dhamana ya ardhi ndiyo yataamua mtu kupatiwa mkopo huo au la.

"Na sheria hii inakwenda kuweka uzalendo wa Mtanzania. Nchi kwanza, eeh! Ukikopa fedha kwa ajili ya kilimo, na mikopo hii inatolewa na benki za nje ya nchi ndiyo maana nikakudokezea tu kwamba kuna Watanzania wamekwenda kukopa nje ya nchi, tena mikopo mikubwa, lakini hawajaboresha lolote katika ardhi ambayo wameikopea," alisema.

"Sheria hii (mpya) ni nzuri, ni moja ya sheria za kizalendo ambayo itatungwa na Bunge la Tanzania. Na huu ni mfululizo wa sheria nzuri kama ile ya madini, inakwenda kulinda rasilimali ya nchi yetu.

"Labda nikwambie tu kwamba wapo Wakenya wamechukua mashamba yetu na kwenda kuyawekea dhamana kwenye benki zao za Kenya.

"Kwa hiyo sheria hii inakwenda kusaidia japokuwa sheria ya sasa inasema hata kama kuna ardhi unaimiliki, Wizara ya Ardhi inaweza kukunyang'anya. Wapo Watanzania, wachache sana lakini, ambao wamechukua ardhi yetu na kwenda kuikopea huko nje.

"Sitaki kuongea 'in details' (kwa kina) kwa sababu ni mambo ya kamati, lakini wapo Watanzania na wengine si Watanzania, mfano hao Wakenya, ambao wameweka ardhi yetu kama dhamana nje ya nchi."

Alisema muswada uliofanyiwa kazi na kamati yake utakuwa na sura tofauti na ule uliowasilishwa na serikali kwa kuwa umefanyiwa uchambuzi mkubwa na maeneo mengi yameboreshwa kwa makubaliano kati ya Bunge na serikali.

Alisema kamati yake imeongeza baadhi ya vifungu katika maeneo ambayo yalionekana kuwa na utata au kutotoa tafsiri ya maneno na pia wamepunguza baadhi ya vifungu ambavyo vilionekana vikipitishwa kama ilivyopendekezwa na serikali havitakuwa na maslahi kwa taifa.

"Kwanza kabisa tumeboresha na kuondoa kipengele ambacho kinajumuisha ardhi yote kwa 'security' ya dhamana. Wapo wananchi wetu ambao ardhi yao kule vijijini ambao na maeneo mengine wasiingie katika sheria hii.

Tukaongeza kifungu ambacho kinawaondoa Watanzania wa kawaida," alisema na kuongeza:

"Kwa hiyo, kimsingi marekebisho haya yanakwenda kuwabana wale watu wakubwa ambao siyo miongoni mwetu sisi wa kawaida. Ni wafanyabiashara wakubwa, wanaochukua ardhi yetu kama dhamana halafu hawaendi kufanya lolote.

"Unajua unapokwenda kukopa benki kwenye ardhi yako, kama unakwenda kukopa kwa ajili ya kilimo fulani, basi sheria hii inataka uende ukalime. Hata kama si kwenye eneo lote, ulime sehemu tu halafu fedha uiwekeze maeneo mengine. Sheria hii haizuii kwamba fedha yote iingie kwenye kilimo.

"Tunataka tujiridhishe ile ardhi yako unaitumia kwa ajili ya kilimo? Umeendeleza kilimo? Lakini kama unataka kukopa kwa vitu vingine, unataka kukopa kwa ajili ya ujenzi wa ghorofa, madhumuni ya mkopo lazima yaonyeshwe kwenye maombi yako unayokwenda kuiombea mkopo."

Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )