Loading...

Tuesday, February 6, 2018

Serikali Kuboresha Mafunzo Kwa Watu Wenye Ulemavu

Na Beatrice Lyimo- MAELEZO, DODOMA
Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuboresha Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi vya Watu wenye Ulemavu ili kuwawezesha kuajiriwa na kujiajiri na kupata ujuzi mbadala wa kumudu maisha yao.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Walemavu) Stella Ikupa jana Mjini Dodoma  wakati akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo Magharibi Mhe. Oscar Mukasa lililohusu umuhimu wa kuwatazama vijana wenye ulemavu mbalimbali kwa namna ya kipekee.

Mhe. Ikupa amesema kuwa Serikali inatambua Vijana wenye ulemavu kuwa ni kundi mojawapo miongoni mwa watanzania wenye ulemavu ambalo linakabiliwa na changamoto mbalimbali.

“Kwa kutambua umuhimu wa kundi hili la watu wenye ulemavu wakiwemo vijana, Serikali iliunda Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu ambalo kazi yake kubwa ni kutoa ushauri kwa Serikali na wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya watu wenye ulemavu juu ya namna bora ya kushughulika na changamoto zao zikihusisha zile za kundi la vijana wenye ulemavu,” alifafanua Naibu Waziri Ikupa.

Aidha, Mhe. ikupa alisema kuwa  Serikali imeendelea kuunda kamati za watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya Mkoa, Halmashauri ya Wilaya, Kata na Mtaa kwa lengo la kuhakikisha masuala ya watu wenye ulemavu yanazingatiwa ili kuondokana na kero mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu Elimu, Afya, Ajira na Mikopo ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Hata hivyo, Naibu Waziri Stella Ikupa amewahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia ipasavyo utekelezaji wa suala hilo ambalo liko kisheria na pia ametoa wito kwa Wakurugenzi hao kuhamasisha walemavu kujiunga kwenye vikundi mbalimbali ikiwemo vikundi vya vijana.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )