Friday, February 9, 2018

Waziri Mkuu: Akiba ya Fedha za Kigeni Imeongezeka na Kufikia dola 5.91 bilioni za Marekani

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema akiba ya fedha za kigeni imeongezeka na kufikia dola 5.91 bilioni za Marekani kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kwa takriban miaka minne kuanzia mwaka 2013 hadi 2016.

Ameyasema hayo leo Februari 9, 2018  bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.

Amesema mbali na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni, pia thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi imekuwa takriban dola 8.695 bilioni za Marekani ikilinganishwa na wastani wa dola 8.828 bilioni za Marekani kwa miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo, amesema utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka ni wa kuridhisha ambapo ukusanyaji wa mapato ulifikia Sh12.95trilioni sawa na asilimia 82.8 ya lengo lililopangwa katika kipindi hicho.

Amesema matumizi ya fedha hizo yameelekezwa katika kugharamia shughuli mbalimbali za Serikali za kuhudumia wananchi na miradi ya kipaumbele ambayo ni kuanza kwa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa.

Pia kugharamia mpango wa elimumsingi bila malipo, kugharamia mpango wa ununuzi wa dawa, vifaatiba na vitendanishi na utekelezaji wa miradi ya usambazaji maji vijijini na mijini na usambazaji wa umeme vijijini kupitia REA.

Miradi mingine ni ununuzi wa meli za abiria na mizigo katika maziwa, ukarabati na ujenzi wa baadhi ya viwanja vya ndege na kujenga na kuendeleza maeneo ya uwekezaji wa viwanda katika mikoa mbalimbali nchini.

“Hakika kwa mafanikio haya tuna kila sababu ya kumpongeza Rais John Magufuli kwa uongozi wake mahiri na juhudi anazofanya za kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma muhimu na maendeleo ya haraka,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kuwa inatekeleza ahadi zake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2017/2018 yanafikiwa kwa kiwango kikubwa.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha na kujenga misingi na mifumo imara ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kuwa na mapato endelevu kwa ajili ya kugharamia matumizi yake.

Vilevile, kuwa na usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato ambao utasaidia kupanua wigo na kudhibiti ukwepaji wa kodi kupitia urasimishaji wa shughuli za uchumi kwa kuwezesha ukuaji wa biashara katika sekta ndogo na za kati ambazo ndiyo mihimili ya kuzalisha ajira na kukuza uchumi.

Akizungumzia kuhusu viashiria mbalimbali vya kiuchumi, Waziri Mkuu amesema vinaonyesha kwamba hali ya uchumi ni nzuri na pato la Taifa katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2017 lilikua kwa wastani wa asilimia 6.8.

“Hali hii inaashiria kwamba tuna matarajio makubwa ya kufikia lengo la mwaka la ukuaji wa asilimia 7.0. Sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji huo ni habari na mawasiliano, uchimbaji madini, biashara, ujenzi na uzalishaji viwandani,” amesema.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )