Saturday, March 10, 2018

Godbless Lema: Uhusiano Usioridhisha kati ya wabunge na viongozi wa Serikali unakwamisha shughuli za maendeleo.

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema uhusiano usioridhisha kati ya wabunge na viongozi wa Serikali unakwamisha shughuli za maendeleo.

Mbunge huyo ameshauri itafutwe suluhu ili kurejesha mahusiano mazuri baina ya makundi hayo.

Akizungumza leo Machi 10, 2018 katika  kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Arusha, Lema amesema kama hakuna mahusiano mazuri kwa viongozi si rahisi kuwapatia wananchi maendeleo.

"Hili ni suala la utawala bora, leo hii kuna watendaji wa Serikali wanaogopa hata kupiga picha na wabunge, hasa wa upinzani. Jambo hili linapaswa kuondolewa kwani lina athari katika jamii,” amesema Lema.

Amesema wabunge wana nafasi ya kuchochea maendeleo ya wananchi na kuondoa kero zao, kwamba kuna wakati kiongozi wa serikali kutokana na sababu za kiitifaki hawezi kupeleka hoja moja kwa moja kwa viongozi wa juu lakini mbunge anaweza.

"Tufanye kazi pamoja, leo hii tunapitisha bajeti ya mkoa lakini kama hatuna mahusiano mazuri baina yetu, sisi kama viongozi sidhani kama tutafanikiwa,” amesema.

Akijibu hoja hiyo ya Lema Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta amesema anaamini viongozi wa Serikali wanajua wajibu wao wa kufanya kazi na wadau mbalimbali.

"Utawala bora ni pamoja na kufanyakazi pamoja na nina imani hili linafanyika lakini kama kuna watu wanatengwa hilo ni jambo la watu binafsi,” amesema.

Hata hivyo, Kimanta ametaka viongozi kufanya kazi ya kutatua kero za wananchi na kuachana na mambo ya siasa kwani chaguzi tayari zimepita sasa ni wakati wa kufanyakazi.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )