Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Monday, March 19, 2018

Jeshi La Magereza Kuja Na Mkakati Wa Kulisha Wafungwa

Mkuu wa Magereza nchini, Kamishna Jenerali Dk. Juma Malewa, amesema Jeshi hilo limeanza kufanyia kazi agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha wanajitosheleza kwa chakula na kulisha wafungwa.

Amesema hatua hiyo itaondoa utaratibu wa wafungwa kupelekewa chakula kutoka nje, kwa kuwa watakuwa wanakula wanachokizalisha wakiwa magerezani.

Dk. Malewa alisema hayo katika mkutano wa maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka maeneo mbalimbali kuweka mkakati wa namna ya kufanikisha agizo hilo la Rais alilolitoa akiwa mkoani Dodoma hivi karibuni.

Rais Magufuli alilitaka jeshi hilo kuhakikisha linawatumia wafungwa kuzalisha chakula kwa ajili ya kuwalisha badala ya kutegemea ruzuku ya serikali kwa chakula.

Alisema kwa sasa Jeshi hilo lina uwezo wa kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 30, kutokana na vifaa vichache vilivyopo, lakini wanatarajia kupokea na kuongeza vifaa zaidi yakiwamo matrekta ili kuongeza nguvu zaidi ya uzalishaji na kufikia asilimia 100 ya kujitosheleza kwa chakula.

“Zoezi hili halitawezekana kutekelezwa kwa haraka sana, itatuchukua kama miaka miwili hadi mitatu kulifanikisha, lakini kwa kutumia nguvu kazi tuliyonayo na vifaa, tutamudu kulitekeleza,” alisema Kamishna Jenerali wa Magereza.

Malewa alibainisha mkakati wa kuhakikisha Magereza inatumika kama chuo cha mafunzo kwa kuwafundisha wafungwa mbinu mbalimbali za kilimo ili wote watumike vyema na kwa ufanisi katika kuboresha sekta ya kilimo.

Hata hivyo, alikiri kuwapo changamoto ya nguvu kazi kama baadhi ya wafungwa wakiwamo waliohukumiwa kunyongwa na mahabusu ambao kisheria hawapaswi kuwa nje ya Magereza, ingawa wanakula magerezani.

Kuhusu agizo la Rais la kuitaka Magereza kuwa sehemu ya ukuzaji wa uchumi kupitia sekta ya viwanda, alisema hilo wameanza kulitekeleza kivitendo kwa kuanzisha kiwanda cha sukari katika Gereza la Mbigiri, kinachojengwa kwa ubia kwa kushirikiana na mashirika ya Hifadhi za taifa ya NSSF na PPF pamoja na kiwanda cha viatu kilichopo Magereza Karanga mkoani Kilimanjaro na kwamba kinajengwa kingine hivyo kuwa viwili eneo moja.

“Tumeshapata oda za ndani na nje ya nchi, na tukishafunga mashine zaidi za kisasa, tutazalisha viatu kwa wingi sana,” Alisema Dk. Malewa.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro, Mzee Ramadhani Nyamka, alisema wamejipanga kutekeleza agizo la Rais kwa kuzalisha kwa wingi, kwani Morogoro ina Magereza 12 na mengi yanajihusisha na uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Nyamka alisema kutokana na kuwa na ardhi yenye rutuba, maji mengi na miundombinu yote muhimu ya kilimo, wanaamini wataweza kufanikiwa.

“Katika Magereza ya Morogoro niseme nguvu kazi inajitosheleza, kwani hatuna wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, kwa hiyo tutatumia fursa ya Morogoro kama ghala la Taifa la chakula kulima kwa bidii tujitosheleze na ziada tuhudumie maeneo mengine, yakiwamo mashule,” alisema Nyamka.

Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Ramadhani Mkele ambaye ni Mkuu wa Gereza Kuu la Arusha, alisema pamoja na changamoto hiyo ya wafungwa waliohukumiwa kunyongwa kuathiri nguvu kazi, bado wakipata vitendea kazi watafanya makubwa zaidi kwenye sekta ya kilimo.

Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )