Wednesday, March 7, 2018

LHRC wafafanua hoja za NEC dhidi ya tamko la asasi za Kiraia

TAARIFA KWA UMMA
UFAFANUZI WA HOJA ZA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI (NEC) DHIDI YA TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimepokea barua Kumb. Na. BA.71/75/01/124 ya tarehe 22 February 2018 kutoka kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi Ndugu Kailima Ramadhani na kupitia kwa umakini mkubwa hoja za Tume Ya Uchaguzi dhidi ya tamko lililotolewa na umoja wa Asasi Za Kiraia, chini ya Jukwaa la Wakurugenzi wa AZAKI, Februari 21, 2018 kuzungumzia hali ya usalama wa raia, haki za binadamu na utawala wa sheria hapa nchini.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kama moja ya asasi zinazounda umoja wa AZAKI hizo kimelazimika kujibu hoja hizo kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika tamko lake lililotolewa Ijumaa Februari 23, 2018 imekituhumu moja kwa moja Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kupitia kwa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi, Bw. Paul Mikongoti, kwa kutoa tamko lenye tuhuma za kupotosha baadhi ya mambo kupitia tamko hilo la umoja wa AZAKI.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapenda kutanguliza pongezi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kupitia hoja pamoja na mapendekezo yaliyotolewa na asasi za kiraia nchini na hata kutoa kasoro za uwasilishaji wa baadhi ya hoja hizo. 

Hata hivyo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapenda kuikumbusha Tume kwamba, tamko husika halikutolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu bali tamko hilo lilitolewa na Umoja wa AZAKI chini ya Jukwaa la Wakurugenzi wa AZAKI.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilishiriki kwenye tamko hilo kama mwanachama wa AZAKI kwa kutambua wazi kuwa lengo la tamko hilo ni kuimarisha hali ya haki za binadamu na demokrasia nchini na si vinginevyo. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapenda kuitoa wasiwasi Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa hakuna maslahi tofauti wala upotoshaji wa makusudi katika utoaji wa tamko hili.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinakiri kufahamu kwa kina sheria na kanuni zinazoratibu chaguzi na kinatambua kwamba lengo la AZAKI haikuwa kubeza wala kuvunja kanuni hizo bali kutoa mapendekezo kwa ajili ya maboresho ya chaguzi na hatimaye kuimarisha demokrasia nchini Tanzania.

Hata hivyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimesikitishwa na kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumshambulia moja kwa moja Bw. Paul Mikongoti licha ya ukweli kwamba, Bw. Paul Mikongoti alikiwakilisha Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kama mwanachama wa umoja huo wa AZAKI. 

Kituo kinapenda kuifahamisha Tume kuwa tamko hili la AZAKI lilisomwa na wakurugenzi tofauti maeneo tofauti nchi nzima na hivyo haikuwa busara kwa Tume kumshambulia moja kwa moja Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wala Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa ubinafsi wake.

Ingawa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikuwa sahihi kukituhumu Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Paul Mikongoti, bado Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeonelea ni busara kufafanua hoja zilizotolewa na umoja wa AZAKI kama ifuatavyo:

1. Kuhusu kituo cha televisheni cha ITV kuadhibiwa na kutakiwa kuomba radhi kwa kurusha habari za kuibwa kwa sanduku la kura

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapenda kuijuza Tume ya Uchaguzi kuwa kilikubaliana na hoja hii iliyotolewa na umoja wa AZAKI kwa kuzingatia misingi ya uhuru wa vyombo vya habari kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba Tanzania inayotoa haki kwa kila Mtanzania pamoja na vyombo vya habari kutafuta na kupokea habari mahali popote pale bila kujali mipaka ya nchi.
 
Hata hivyo baada ya kupitia hoja hii kama ilivyofafanuliwa na Tume ya Uchaguzi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaishauri Tume kuboresha kanuni za usimamizi wa uchaguzi ili kutokuweka mipaka kwa vyombo vya habari kwa kuzingatia kwamba vyombo vya habari vinatoa taarifa kwa maslahi ya umma.

2. Kuhusu mashirika mbalimbali kunyimwa kibali cha uangalizi wa uchaguzi

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilikubaliana na hoja hii kwa kuzingatia malalamiko yaliyotokana na AZAKI ya PACUSO ambao walikiri kupata majibu kutoka Tume kuwa tayari nafasi zimejaa.
Hata hivyo baada ya kupitia hoja hii ya Tume, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaishauri Tume ya Uchaguzi kuboresha utaratibu wa maandalizi kuelekea uchaguzi ili kutoa nafasi kwa asasi zenye lengo la kufanya uangalizi kufurahia haki hiyo bila kuhisi uwepo wa kuzuiliwa. Moja ya maboresho hayo ni kuweka muda wa kutosha wa kutuma maombi na kuweka nguvu katika kufikisha taarifa kwa mashirika na wadau wengine. Kufuatia ukweli kwamba Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ndio asasi pekee iliyopata kibali kutazama uchaguzi huu, hili lilipelekea butwaa kwa umoja wa AZAKI kwa kulinganisha na chaguzi zilizopita.

3. Tume kuweka utaratibu mpya unaowataka watazamaji kuwasilisha taarifa hizo ili zikaguliwe, kuangalia yaliyomo na kuridhiwa na Tume ikiipendeza.

Katika hoja hii, Kituo kinaungana na AZAKI kuhoji umuhimu wa utaratibu ulioanzishwa na Tume mwaka 2015 wa AZAKI kusubiri hadi Ripoti ya awali ya uangalizi iwasilishwe kwa Tume, na Tume kukiri kupokea ripoti hiyo ndipo AZAKI zinazoangalia uchaguzi kuweza kutoa kwa umma taarifa za uangalizi. AZAKI zimeonelea kwamba utaratibu huu unafifisha misingi ya uhuru wa asasi za kiraia katika uangalizi wa uchaguzi.

Utaratibu huu pia umelalamikiwa kwa kuzingatia kuwa Tume haijaweka muda maalumu ambao itatumia kabla ya kukiri kupokea ripoti ya uchaguzi.
 
Utaratibu huu umelalamikiwa na AZAKI kuwa kwa upande mwingine unaondoa dhana ya AZAKI kuwa vyombo huru vya uangalizi wa uchaguzi.

Mwisho Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaishauri Tume ya Uchaguzi kuzishirikisha asasi za kiraia na wadau wengine muhimu katika maboresho ya sheria, kanuni na taratibu zinazoratibu utendaji wa Tume na usimamizi wa chaguzi kwa lengo la kuboresha na kuimarisha demokrasia nchini Tanzania. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaisihi Tume ya Uchaguzi bila kujali madhaifu katika uwasilishaji, kufanyia kazi changamoto zinazoibuliwa na wadau kwa lengo la kujenga Jamii yenye Haki na Usawa.

Imetolewa na;

Naemy Sillayo (Wakili)
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )