Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Friday, May 4, 2018

Salum Mwalimu Afungua Kesi Kupinga Ushindi wa Maulid Mtulia wa Kinondoni

Ubunge wa Maulid Mtulia wa Kinondoni (CCM), umewekwa rehani na aliyekuwa mpinzani wake, Salum Mwalimu (Chadema) aliyefungua kesi akipinga matokeo ya uchaguzi mdogo uliofanyika Februari 17.

Mtulia aliibuka mshindi kwa kura 30,313 dhidi ya 12,353 alizopata Mwalimu. Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na Mtulia kujivua ubunge wa jimbo hilo akiwa CUF na kujiunga na CCM iliyompitisha kugombea.

Mwalimu amefungua kesi dhidi ya Mtulia; msimamizi wa uchaguzi ambaye ni mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Mbali ya kesi ya msingi namba 129 ya mwaka 2018, Mwalimu amefungua maombi ya kusamehewa au kupunguziwa kiwango cha fedha anachopaswa kukiwasilisha mahakamani kama dhamana kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi hiyo.

Katika kesi ya msingi, Mwalimu anaiomba mahakama itengue matokeo na itamke kuwa uchaguzi ulikuwa batili, pamoja na mambo mengine akidai uligubikwa na kasoro nyingi na mwenendo mbaya.

Anadai Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson wakati wa kampeni alitoa kauli za ubaguzi.

Katika hati ya madai , Mwalimu anadai msimamizi wa uchaguzi alishindwa kutoa fomu (kiapo cha siri) kwa mawakala wake wa vituo vya kupigia kura siku saba kabla ya uchaguzi kinyume cha Kanuni za Uchaguzi za mwaka 2015.

Anadai bila sababu za msingi, msimamizi wa uchaguzi alikataa na alishindwa kuteua mawakala mbadala wa vituo vya kupigia kura licha ya kuwasilisha kwake majina ya mawakala hao yaliyopendekezwa.

Pia, anadai aliweka masharti mengine kwa mawakala wa vituo vya kupigia kura akiwataka kuwa na kadi za utambulisho na barua za utambulisho kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi, aliloliweka siku ya upigaji kura.

Anadai msimamizi alishindwa kuhakikisha usalama wa masanduku ya kupigia kura, hivyo kusababisha moja katika kituo cha kupigia kura namba 3 kwenye Mtaa wa Idrisa, Kata ya Magomeni kuhamishwa na watu wasiojulikana wakati wa upigaji kura na kurejeshwa nusu saa baadaye.

Mwalimu anadai timu ya kampeni ya Mtulia iliyomhusisha Dk Tulia ilitoa maneno ya ubaguzi na yaliyompa haki isiyo sawa mpinzani wake.

Anadai maneno yaliyotolewa na Dk Tulia ni “Mkimchagua Mtulia nitampanga kukaa karibu na waziri mkuu.”

Mwalimu anadai mtiririko wa kasoro, ukiukwaji wa sheria na utaratibu uliathiri matokeo ya uchaguzi na demokrasia.

Mwanasiasa huyo anaiomba mahakama ibatilishe matokeo yaliyompa ushindi Mtulia akidai uchaguzi haukuwa huru na wa haki, hivyo ni batili.

Katika kesi za uchaguzi kila anayefungua kupinga matokeo anapaswa kuwasilisha mahakamani Sh5 milioni kama dhamana ya usikilizwaji wa kesi kwa kila mdaiwa. Kwa kawaida kesi za uchaguzi wadaiwa wa msingi huwa watatu; mbunge aliyeshinda, msimamizi wa uchaguzi aliyemtangaza mshindi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kama ilivyo kwa Mwalimu, anapaswa kuwasilisha mahakamani Sh15 milioni kama dhamana ya usikilizwaji wa kesi.

Hata hivyo, Sheria ya Uchaguzi inatoa nafasi kwa mtu ambaye anadhani hana uwezo wa kupata kiasi hicho cha fedha kuwasilisha maombi akiomba kusamehewa zote au kupunguziwa kiwango. Kama mahakama itajiridhisha kuwa hana uwezo basi inaweza kumsamehe au kumpunguzia kiwango na kumpangia itakachoona inafaa.

Mwalimu amewasilisha maombi mahakamani akiomba asamehewe kabisa au impunguzie akidai si mbunge, hivyo hana uwezo wa kuweka kiasi hicho cha fedha.

Mashauri hayo (kesi ya msingi pamoja na maombi), yaliyopangwa kusikilizwa na Jaji Ignas Kitusi yalitajwa mahakamani jana. Jaji Kitusi ameelekeza Mtulia apewe nyaraka za mashauri hayo baada ya kubaini hajapewa.

Mwalimu aliwakilishwa na wakili Alex Masaba, huku msimamizi wa uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Benson Hoseah. Mashauri hayo yaliahirishwa hadi Mei 14 yatakapotajwa.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

taboola apo chini
....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )