Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Monday, June 11, 2018

Askofu Mkuu Avunja Ukimya.....Asema KKKT Hawakukurupuka Kuandika Waraka Wao

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Onael Shoo amesema waraka uliotolewa na maaskofu wa kanisa hilo haukuwa na nia mbaya na wala hawakukurupuka kuuandika.

Askofu Dk. Shoo alitoa ufafanuzi huo jana wakati wa ibada uzinduzi wa Dayosisi ya Magharibi Kati ya kanisa hilo mjini Tabora ya kumsimika Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk. Isaac Kissiri na msaidizi wake, Mchungaji Newton  Maganga, iliyohudhuriwa na maaskofu wote wa kanisa hilo.

Alisema kanisa linaunga mkono jitihada zote zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema    kanisa hilo  halina ugomvi na kiongozi yeyote   wa Serikali  ya Rais Magufuli.

Kuhusu waraka uliotolewa wakati wa Sikukuu ya Pasaka   mwaka huu, alisema haukuwa wa kukurupuka na haukutolewa kwa lengo baya dhidi ya Serikali  kama    baadhi ya watu wanavyoupotosha.

“Naomba  kila mpenda amani na maendeleo ya nchi hii aelewe hivyo, waraka huu haukuwa na nia mbaya na Serikali,”alisema Dk. Shoo.

Alisema lengo la waraka huo lilikuwa ni   kufikisha ujumbe wa kanisa kwa Serikali  iweze kuutafakari na kuufanyia kazi na haukuwa na lengo jingine tofauti.

“Kama kuna sehemu tulieleweka vibaya tuko tayari kuomba radhi kwa nia njema  kudumisha ushirikiano mzuri na Serikali.

‘Namshukuru  Rais wetu Magufuli kwa kuelewa dhamira yetu, ila wapo baadhi ya watu ndani ya kanisa na nje ya kanisa wasio na nia njema wanaotaka kutuchonganisha na Serikali, watu wa namna hii wasifumbiwe macho, wana agenda binafsi’, alisema Dk. Shoo.

Alisema ndiyo maana maaskofu wote wa kanisa hilo na waumini wao wako kitu kimoja, hawana tofauti zozote.

Kiongozi huyo wa KKKT alionya  kuwa  mtu anayeendelea kushabikia mambo yanayovuruga amani ndani ya kanisa hilo anakiuka kiapo chake cha utumishi wa Mungu.

Alisema maaskofu wataendelea  kushirikiana na Serikali kudumisha amani na utulivu wa nchi na hawako tayari kuona mtu yeyote anatumia jina la kanisa hilo vibaya kwa matakwa yake binafsi   kuharibu taswira ya kanisa na Serikali.

“Hatuko tayari kuona mtu anaharibu ushirikiano wetu na Serikali kwa sababu umejengeka muda mrefu, kanisa litachukua hatua kali dhidi yake,”alisema Dk. Shoo.

Alimshukuru Rais Magufuli kukubali mwaliko wao na kumtuma Samia   kujumuika nao katika ibada na kuomba awafikishie shukrani za kanisa.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )