Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Wednesday, June 13, 2018

Kamishna Mkuu Wa TRA Awashukuru Wafanyabiashara Jijini Dodoma

Na Veronica Kazimoto
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere amewashukuru wafanyabiashara jijini Dodoma kwa mchango wao wa kulipa kodi na kuiwezesha Serikali kutekeleza wajibu wake wa kukuza uchumi na kutoa huduma mbalimbali za jamii hapa nchini.

Akizungumza wakati akifuturisha wafanyabiashara na wafanyakazi wa TRA katika ukumbi wa LAPF jijini hapa, Kichere alisifia uhusiano mzuri uliopo kati ya wafanyabiashara hao na ofisi ya TRA Mkoa wa Dodoma.

"Nachukua nafasi hii kuwashukuru wafanyabiashara wa Dodoma kwa kuwa walipakodi wazuri na kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu na ofisi yetu ya TRA hapa mkoani Dodoma ambapo kutokana na uhusiano huu uliopo, tunapata urahisi wa kutekeleza jukumu letu la kukusanya mapato ya Serikali kwa manufaa ya watanzania wote," alisema Kichere.

Kichere amewaahidi wafanyabiashara hao kuwa, TRA itaendelea kudumisha ushirikiano huo na kukaribisha mazungumzo ya pamoja na viongozi wa TRA mkoani hapa ili kufikia muafaka wa masuala mbalimbali yanayohusu kodi badala ya kulalamika mitaani bila kupata suluhisho.

Aidha, Kamishna Mkuu Kichere amewahimiza wafanyabiashara hao kuendelea kulipa kodi mbalimbali kwa wakati kwani kodi hizo hutumika katika kujenga uchumi wa nchi na kutoa huduma mbalimbali za jamii ikiwa ni pamoja na huduma za afya, maji safi na salama, elimu, kulipa mishahara ya watumishi wa Umma, miundombinu ya barabara na umeme.

"Nachukua fursa hii kutoa rai kwenu wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi zote kwa wakati ikiwa ni pamoja na Kodi ya Majengo na  Kodi ya Mapato awamu ya pili ambapo mwisho wa kulipa kodi hizi ni tarehe 30 Juni, mwaka huu. Kodi nyingine ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo hulipwa tarehe 20 ya kila mwezi.  Hivyo, uhiari wenu wa kulipa kodi hizi kwa wakati ndio chachu ya kujenga uchumi wetu na kuharakisha kutoa huduma za jamii kwa watanzania wote", alisema Kichere.

Naye Katibu Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Dodoma ambaye pia ni Katibu wa Sekta Binafsi mkoani hapa Idd Senge amesema kwamba, sekta binafsi itaendelea kushirikiana na TRA kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanalipa kodi kwa wakati ili kuepuka faini ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya biashara zao.

"Sisi kama wafanyabiashara wa hapa mkoani Dodoma tutaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania na pale patakapotokea sintofahamu yoyote tutafanya mawasiliano na viongozi wa TRA ili kupata muafaka wa pamoja," alieleza Senge.

Mamlaka ya Mapato Tanzania imejiwekea utaratibu wa kufuturisha wafanyabiashara na wafanyakazi wake kila ifikapo Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa lengo la kumshukuru Mwenyezi Mungu katika shughuli mbalimbali wanazozifanya hususani za ukusanyaji mapato ya Serikali.

Mwisho.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )