Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Wednesday, June 20, 2018

Ufaransa Kuipatia Tanzania Mkopo Nafuu Wa Sh. Trilioni 1.3 Kusaidia Sekta Za Maji, Nishati Na Usafirishaji

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
SERIKALI ya Ufaransa kupitia Shirika lake la  Maendeleo (AFD), itaipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa Euro milioni  500, sawa na takriban Shilingi trilioni 1.3, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maji, Nishati na Usafirishaji, kupitia Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo (2017-2021).

Hayo yamesemwa Jijini Dodoma, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bw. Remy Rioux, ambapo ujumbe wa Tanzania na Ufaransa umejadili namna ya kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili uliodumu kwa zaidi ya miaka 58.

"Kupitia makubaliano hayo, AFD itakuwa inatoa Euro milioni 100 kila mwaka, sawa na karibu shilingi bilioni 267 kwa kipindi cha miaka mitano, kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu" Alisema Bw. James.

Bw. James amesema kuwa fedha hizo ni tofauti na  Euro milioni 600 ambazo shirika hilo limeipatia Tanzania kama msaada na mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa hapa nchini ukiwemo Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Ziwa Victoria unaohusisha mikoa ya Mwanza, Bukoba na Musoma ambapo Serikali hiyo ilitoa Euro milioni 45.

Miradi mingine inayofadhiliwa na Shirika hilo ni pamoja na Mradi wa Kuendeleza Sekta ya Maji Awamu ya Pili (WSDP II), Mradi wa Vituo vya kupoza umeme kupitia TANESCO, na Ujenzi wa njia ya Umeme kutoka Geita hadi Nyakanazi na mingine mingi ambayo kwa pamoja  imefikia thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.055.

Bw. James ameishukuru Serikali ya Ufaransa kupitia AFD kwa namna inavyoshiriki katika kuleta maendeleo ya nchi na watu wake kupitia ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuiomba iendelee kuangalia maeneo mengine ya vipaumbele vya taifa ikiwemo kilimo, elimu na miundombinu mingine.

Akizungumza katika kikao hicho kilichowashirikisha pia viongozi waandamizi wa pande zote mbili, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bw. Remy Rioux, amesema kuwa Shirika lake litaangalia namna ya kutoa fedha zingine kwa ajili ya miradi mipya ya kipaumbele iliyoainishwa na Katibu Mkuu-Hazina, Bw. Doto James, ukiwemo mradi mkubwa wa Bwawa la Maji wa Farkwa utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha lita za ujazo 37,000 kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Jiji la Dodoma, uliopangwa kugharimu Dola la Marekani milioni 420.

"Tuko tayari pia kufadhili ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme jua katika mkoa wa Shinyanga na tutakamilisha majadiliano yetu na Wizara ya Nishati ili kufadhili mradi wa kuunganisha umeme kati ya Tanzania na Zambia pamoja na kushiriki kwa kutoa fedha katika Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza" aliongeza Bw. Rioux.

Alisema pia kuwa Shirika lake liko tayari kuelekeza nguvu zake katika kukuza sekta zingine ikiwemo Sekta ya utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa-TANAPA, Shirika la Simu Tanzania-TTCL, na Taasisi nyingine ambazo serikali itaona zina umuhimu wa kupata rasilimali fedha kutoka AFD kwa ajili ya kusukuma haraka gurudumu la maendeleo ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kuwa Shirika lake ambalo juzi limesherehekea miaka kumi tangu lianze kufanya shughuli zake hapa nchini, limeamua kuanzisha Ofisi yake ya Kudumu nchini Tanzania badala ya kutegemea Ofisi yake iliyopo Nairobi Kenya, baada ya kuridhika na kutambua jitihada kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano za kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

"Tumeamua kufanya hivyo ili tuweze kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali katika azma hiyo ya kuifanya Tanzania nchi yenye uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025" alisisitiza Bw. Rioux.

Uhusiano wa Tanzania na Ufaransa ulianza tangu miaka ya 1960 na ukaimarishwa zaidi mwaka 1979, ambapo kwa mara ya kwanza, Serikali ya nchi hiyo iliipatia Tanzania mkopo wa kiasi cha fedha za Ufaransa, faranga milioni 361, kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (Julius Nyerere).

Mwisho
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )