Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Thursday, June 21, 2018

Wakurugenzi Halotel, Zantel Wahukumiwa Jela miaka 40 Au Faini Milioni 139

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu watu sita na kampuni mbili, wakiwamo wakurugenzi watendaji wa kampuni za simu za mkononi, Le Van Dai (35) wa Halotel na Sherif El-Barary wa Zantel,kulipa faini ya Sh. milioni 139 au kwenda jela miaka 40 baada ya kukiri tuhuma za uhujumu uchumi.

Washtakiwa wote walikiri jana tuhuma zilizokuwa zinawakabili zikiwamo za kula njama, kuingiza, kufunga mitambo, matumizi ya laini za simu bila usajili wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 1,131,936,000.

Hukumu hiyo ilitolewa na mahakama hiyo chini ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Kevin Mhina, baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka yao 12 na kukiri.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na mawakili wa serikali Jacqueline Nyantori na Batilda Mushi.

Nyantori aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni, Lei Cao maarufu kama Peter (28), Huang Yu Meng (27), Msimamizi wa Biashara wa Halotel Zanzibar, Jimmy Mosha (26), Meneja Masoko wa Halotel, Willy Ndoni (29), Kampuni ya Viettel Tanzania Ltd maarufu kama Halotel iliyoko Kinondoni na Kampuni ya Zanzibar Telecommunication PLC, maarufu kama Zantel, iliyoko Msasani, Dar es Salaam.

Alidai katika shtaka la kwanza, kati ya Januari Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu nchini Tanzania, mshtakiwa wa kwanza hadi wa sita, walikula njama ya kutenda kosa la kutumia huduma za mawasiliano kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili, kati ya Mei Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu, katika jengo la Spring lililoko Mbezi mshtakiwa wa kwanza hadi wa sita, kwa pamoja walifunga mitambo ya mawasiliano kwa njia ya udanganyifu na kujipatia huduma za mtandao wa Halotel na Zantel bila kibali cha TCRA .

Shtaka la tatu, nne, tano na sita, kati ya Januari Mosi na Desemba 31, 2017, Aprili 30, mwaka huu jijini Dar es Salaam, mshtakiwa wa tatu na wa nne, waliingiza nchini, waliifunga na kuendesha mitambo ya mawasiliano kwa kuunganisha na kampuni hizo za simu bila kibali cha TCRA.

Shtaka la nane, kati ya Mei Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu katika jengo la Spring City, mshtakiwa wa tatu na wa nne, walikutwa wakitumia laini za simu za mkononi zisizosajiliwa na TCRA 281,272 za Halotel na 11,920 za Zantel.

Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shtaka la 10 kuwa kati ya Mei, 2017 na Aprili 30, mwaka huu katika matawi ya Zantel ya Dar es Salaam, mshtakiwa wa pili na wa nane walitumia kwa makusudi laini za simu 11,920 zisizokuwa na usajili wa TCRA.

Shtaka la 11 na 12, kati ya Mei Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu washtakiwa waliisababishia serikali hasara ya Sh. 1,131,936,400.

Kwa mujibu wa mashtaka yanayowakabili washtakiwa kisheria kesi hiyo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote hadi upelelezi utakapokamilika itasikilizwa Mahakama Kuu Tanzania, Divisheni ya Uhujumu Uchumi au kwa kibali maalumu kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Aidha washtakiwa walikiri maelezo yote ya awali.

Hakimu Mhina aliahirisha kesi hiyo saa 8:05 na kurejea saa 8:30 kuwasomea washtakiwa hukumu.

Hakimu alisema katika shtaka la kwanza na la pili, washtakiwa wanatakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 20 au jela miaka sita na kwa kosa la tatu mpaka la sita, walipe faini ya Sh. milioni 20 au kwenda jela miaka minane.

Kwa kosa la saba mpaka la 10, aliamuru walipe faini ya Sh. milioni 22 au kwenda jela miaka 12 na kwa kosa la 11 na la 12, walipe faini Sh. milioni 20 au kwenda jela miaka 14.

Pia mahakama hiyo ilisema washtakiwa walipe fidia ya zaidi ya Sh. bilioni moja wanayodaiwa kuisababishia serikali hasara na mali zote ikiwamo mitambo na kadi za simu wanazodaiwa kukutwa navyo, washtakiwa viteketezwe.

Pia hakimu aliuamuru upande wa Jamhuri uwarejeshee washtakiwa hati zao za kusafiria, vibali vya kuishi nchini na leseni za biashara.

Vigogo hao walilipa faini kuepuka kifungo, kasoro washtakiwa Lei Cao na Huang Meng ambao walipelekwa gerezani.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )