Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Saturday, June 23, 2018

Zitto Kabwe Afunguka Mazito...." Ni makosa makubwa tunakwenda kuyafanya"

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amesema hali mbaya ya uchumi iliyoko nchini na matatizo ya kibajeti ni matokeo ya makosa yaliyofanyika katika bajeti ya mwaka 2016/17 baada ya serikali kuongeza kodi kwenye maeneo mbalimbali, hususan utalii.

Vile vile, amesema endapo sekta ya utalii, zao la korosho na Bandari ya Dar es Salaam vitaendelea kuchezewa, kiwango cha kubadilishia fedha kitafika Sh. 5,000 hadi 6,000 kwa Dola moja.

Zitto alitoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma jana alipokuwa anachangia mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017.

“Matatizo yote ya kibajeti na ukwasi wa fedha tulio nao hivi sasa ni kutokana na makosa yaliyofanyika mwaka 2016/17 baada ya serikali kuongeza kodi kwenye huduma za utalii," Zitto alisema na kueleza zaidi:

“Ndiyo maana bajeti hii na ya mwaka jana imepanda kwa asilimia mbili tu. Serikali irekebishe makosa haya kwa sababu tangu kodi imepandishwa kwenye utalii, kasi yetu ya kuongeza utalii imezidi kushuka.

“Huko nyuma utalii ulikua kwa asilimia 12 lakini sasa hivi ni asilimia tatu. Nataka niwaambie sasa hivi ukicheza na utalii, ukicheza na Bandari ya Dar es Salaam, ukicheza na zao la korosho, 'exchange rate' (kiwango cha kubadilisha fedha) kitafika mpaka Sh. 5,000 na 6,000.

“Hii ni kwa sababu sekta hizi zinatuingizia fedha za kigeni. Napendekeza ile VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) kwenye utalii iondolewe."

Akizungumzia kuhusu mfumo mpya wa stempu za kielektroniki (ETS), Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo alisema utaongeza gharama kwa wananchi kwa sababu bei ya vinywaji kama vile maji na soda itaongezeka, lakini akasisitiza kuwa ukisimamiwa vizuri mapato ya nchi yataongezeka.

Kuhusu kusudio la marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Korosho ili asilimia 65 ya mauzo ghafi yapelekwe kwenye Hazina, Zitto alisema ni makosa makubwa kwa serikali kutaka kuchukua fedha hizo za wakulima.

“Fedha ambayo imetengwa kisheria mmechukua hamjarudisha halafu hapo hapo mnataka kubadilisha sheria ili fedha hizo ziende kwenye Mfuko wa Hazina, hili haliwezekani kabisa,” Zitto alisema.

Katika mjadala huo, Mbunge wa Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka (CCM), alisema kwa sasa serikali inatumia fedha nyingi kulipa Deni la Taifa, jambo ambalo anaamini litakwamisha maendeleo.

“Waziri wa Fedha na Mipango, (Dk. Philip Mpango) tunakuomba utakapokuja hapa kufanya majumuisho, utuletee majibu kwamba tumejisahau wapi," alisema Prof. Tibaijuka.

Naye Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema) aliitaka serikali kukamilisha mradi mmoja baada ya mwingine na kuachana na utaratibu wake wa kuanzisha miradi mipya wakati ya nyuma haijakamilika.

“Tulianza gesi ya Mtwara ambayo ingewanufaisha wananchi lakini serikali imeruka, imeachana na gesi wamekimbilia kwenye mradi wa Stiegler’s Gorge. Hatuna nia ya kupinga huu mradi lakini kwanini tusikamilishe kwanza miradi iliyopo?" Mwambe alihoji.

“Kuhusu zile Sh. bilioni 81 za wakulima wa korosho, nitaongoza wananchi wangu wa Ndanda katika maandamano mpaka serikali itoe hizo fedha kama alivyosema juzi Bwege (Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara -CUF).

“Fedha zetu hawajatupa halafu wanataka kubadilisha sheria ili fedha zote ziende kwao, hatutakubali na wanataka kuwaingiza Watanzania mkenge, hili jambo watuachie sisi wamakonde."

Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), aliunga mkono hoja hiyo akieleza kuwa Dk. Mpango asipotoa Sh. bilioni 81 za Mfuko wa Korosho, wananchi wa kusini hawatamwelewa.

“Mnataka kubadilisha sheria ili fedha mchukue, huu uchumi wa aina gani huu Dk. Mpango? Naomba upeleke fedha za korosho vinginevyo hatutakuelewa maisha yote. Hii habari si ndogo hata kidogo. Hicho chama chenu lazima mjue mnakizika huko kusini," Bobali alisema.

Katika mjadaka huo, Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga (Chadema), aliitaka serikali kupandisha mishahara ya watumishi wa umma kwa kuwa ni muda mrefu haijafanya hivyo ilhali ni matakwa ya kisheria.

Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu (CCM) aliipongeza serikali kwa jitihada zake kukuza uchumi wa Tanzania lakini akakosoa operesheni dhidi ya uvuvi haramu inayofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, akieleza kuwa inapunguza mapato yatokanayo na sekta ya uvuvi.

Advertisement
Loading...
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
==

taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )

Loading...