Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Monday, July 9, 2018

Mahakama Yatupitilia Mbali Ombi la Ruzuku la Chama cha Democratic (DP)

Chama cha Democratic (DP) kimegonga mwamba katika harakati za kutaka kufutwa kwa sheria ya ruzuku kwa vyama vya siasa iliyotolewa kwa ajili maandalizi ya uchaguzi.

DP ilitaka iwapo sheria hiyo haitafutwa, nacho kipewe ruzuku ya Sh100 milioni kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Mahakama ya Rufaa imetupilia mbali maombi ya DP ya marejeo ya uamuzi uliotolewa awali na mahakama hiyo katika rufaa ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotupilia mbali kesi ya msingi kuhusu kufutwa sheria hiyo.

Uamuzi wa majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, Bernard Luanda (kiongozi wa jopo), Augustine Mwarija na Rehema Mkuye ni wa tatu kutolewa kuhusu suala hilo.

Bodi ya wadhamini wa DP, chama kilichoasisiwa na hayati Mchungaji Christopher Mtikila, ilifungua kesi Mahakama Kuu ikiomba kufutwa kwa Sheria ya Ruzuku ya Serikali Namba 11 ya mwaka 1996, ikidai inakiuka Katiba.

Chama hicho kilidai sheria hiyo ni ya kibaguzi kwa kuwa inakinyima ruzuku wakati CCM na CUF vilipewa. Bodi hiyo iliomba DP ipatiwe Sh100 milioni ili kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, kama ambavyo CCM na CUF vilipewa kujiandaa na uchaguzi huo.

Katika hukumu yake, Mahakama Kuu ilitupilia mbali kesi hiyo kutokana na bodi ya DP kutokuwa na hoja za kisheria zenye mashiko mbele ya jopo la majaji watatu walioisikiliza. Baadaye DP ilikata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi huo.

Katika uamuzi dhidi ya rufaa namba 125 ya mwaka 2008 iliyotolewa Agosti 10, 2012 na jopo la majaji-- Eusebia Munuo (kiongozi wa jopo), Bernard Luanda na Sauda Mjasiri-- iliitupilia mbali rufaa hiyo kutokana na kutokuwa na mashiko kisheria. DP ilifungua maombi kutaka Mahakama ya Rufaa hiyo ifanye marejeo ya uamuzi wake.

Akisoma uamuzi wa Mahakama, Naibu Msajili, Amir Msumi alisema wanakubaliana na (wakili wa Serikali kwamba ombi la DP kwa mahakama ni kufungua na kusikiliza upya rufaa yake.

Msajili alisema maombi haya yanafutwa na mwombaji anapaswa kulipa gharama za usikilizwaji.

Mahakama imesema kifungu cha 16 (3) (b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura 258 si cha kibaguzi na hakikiuki Katiba ya nchi.

Korti imesema kifungu hicho kinatumika kwa usawa kwa vyama vyote vinavyotimiza masharti ya kupata ruzuku.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, wakili wa DP, Audax Vedasto aliiomba Mahakama izingatie hoja zao za maandishi akisisitiza kuwa haikutoa uamuzi kwenye hoja za msingi.

Wakili wa Serikali, Mark Mlwambo aliyemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), aliiomba Mahakama izingatie hoja zake za maandishi akisisitiza kuwa, mwombaji anatafuta kufungua upya rufaa kwa kupitia mlango wa nyuma. Alidai bodi ya DP imeibua hoja mpya, hivyo haijakidhi vigezo vya maombi ya marejeo.
Advertisement
Loading...
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
==

taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )

Loading...