Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Thursday, August 23, 2018

Kamati ya Bunge Yatoa Maagizo Mazito Mradi wa Reli ya Kisasa

Wakati  ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ukiendelea, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeagizwa kuwasilisha kwa maandishi mkakati wa upatikanaji wa umeme wa uhakika wa kuendesha treni hiyo kwa Kamati ya Bunge, Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) kabla ya Mkutano wa Bunge la Novemba.

Wabunge hao wametoa agizo hilo kwa TRC kutokana na wasiwasi wao kuhusiana na upatikanaji wa umeme wa kutosha.

Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa kikao cha kamati hiyo, Janet Mbene, baada ya shirika hilo kuwasilisha majibu ya hoja ambazo kamati iliziagiza mara ya mwisho walipokutana na utekelezaji wa majukumu yao tangu ilipoundwa TRC.

Mbene alisema TRC ambayo ndiye msimamizi wa ujenzi huo inatakiwa ioneshe mkakati wake wa kuanza kujiandaa kuhusu umeme utakaotumika kwenye treni hiyo, watumishi watakaofanya kazi, ulinzi na vitu vyote vinavyoendana na uendeshaji wa treni hiyo.

“Treni ya SGR itatumia umeme, hatujaona popote wapi mmeanza mazungumzo na Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) kujua umeme utapatikana vipi na kwa gharama zipi, lazima hivi vitu sasa hivi mvitazame, msisubiri hadi treni ifike na reli imekamilika ndio mnaanza kufanya kazi,” alisema Mbene.

Mbene aliwataka kuwasilisha mkakati wa uboreshaji gani utafanyika kwa reli iliyopo wakati wakiwa wanasubiri SGR.

“Mpango uliopo wa kujenga SGR mpaka Makutupora, lakini reli hii inapaswa kufika Kigoma na Mwanza kwa hiyo tumeagiza waje na mchanganuo unaoonesha jinsi gani hii reli itafika Kigoma na Mwanza,” alisema zaidi Mbene.

Mwenyekiti huyo alisema shirika hilo linaweza kukopa au kuingia ubia kama njia ambazo zipo wazi kwao zitawafanya wawe na fedha za kutosha za kufikisha reli mwisho badala ya kusubiri kutoka serikalini.

“Tayari wanasema kuna wawekezaji wameonyesha nia ya kuwekeza na wapo tayari kuwekeza maeneo ya hiyo reli, sasa tunataka watuletee tuone je, kwa kuwatumia hao huo mpango wa ubia unaweza kuwa na manufaa badala ya kusubiri serikali pekee iwekeze,” alisema.

Pia Mbene alisema mfuko unaotokana na uagizwaji wa bidhaa nje ambapo asilimia 1.5 ya fedha huingia moja kwa moja kwenye miundombinu ya reli ni vyema fedha nyingine itumike kuboresha miundombinu ya reli na SGR iliyopo kwa kuweka mgawanyo sawa.

Kadhalika, alisema kuna fedha zimetoka Benki ya Dunia Dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya ukarabati wa reli ambapo unahusisha madaraja, maeneo ya madaraja na vipande vya reli.

“Musoma-Bukoba, Moshi-Tanga, Mtwara-Mchuchuma, Mpanda-Kaliua, sasa vyote hivi ni vya fedha kutoka benki ya dunia tunachohitaji kujua wana mkakati gani mbadala wa kuhakikisha kuwa ufanisi hautaathirika na tumeagiza haya yote yaletwe bunge la mwezi Novemba,” alisema.

Alisema kumekuwapo na changamoto ya kila mwaka inayojirudia katika kipande cha reli cha Gulwe hadi Kilosa ambapo mvua zikinyesha reli husombwa na kusababisha adha kwa wasafiri.

“Tumeona hii ni kero ambayo inaweza kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, inawezekanaje kila mwaka wanakuwa na mikakati hafifu, kwa hiyo tumeagiza watuletee maelezo ya ufumbuzi wa kudumu kwa maeneo korofi ili kupunguza gharama zinazotokana na ukarabati wa kila siku na usumbufu kwa wananchi wanaotumia treni,” alisema.

Akijibu baadhi ya hoja, Mwenyekiti wa Bodi ya TRC, Prof. John Kondoro, alisema kuna mazungumzo yanaendelea ya upatikanaji wa umeme na vitu mbalimbali yapo katika maandiko.

Aidha, alisema ukarabati mwingi unafanyika na maeneo yameainishwa ambapo kuna baadhi ya njia na madaraja zinakarabatiwa kwa kuwa mtandao wa reli una jumla ya madaraja 400.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

taboola apo chini
....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )