Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Wednesday, August 8, 2018

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini John Shibuda Awataka Wanasiana Kuwa Makini na Kauli Wanazotumia Dhidi ya Rais Magufuli

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini John Shibuda amewashauri viongozi wa vyama vya siasa kuwa makini na matumizi ya lugha wanayotumia pindi wanapotaka kumshauri Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano Dk.John Magufuli.

Wakati huo huo amewahakikishia kuwa Rais Magufuli hawezi kuufuta mfumo wa vyama vingi bali kilichopo anaviimarisha na kwamba ipo siku atazungumzia hilo kwa kina.

Shibuda ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati viongozi wa vyama vya siasa nchini vilipokutana kwa lengo la kujadili mabadiliko ya kikatiba na kisheria kuhusu uchaguzi kabla ya Uchaguzi kuu wa mwaka 2020.

Katika mkutano huo ambao umeandaliwa na Jukwa la Katiba Tanzania (Jukata),Shibuda amesema ni vema wanasiasa wakawa makini katika matumizi ya lugha hasa kwa kuzingatia zama zimebadilika.

Amesema lugha ambazo walikuwa wanazitumia katika awamu zilizopita lazima wanasiasa wajue zama hizi hazina nafasi na hivyo kushauri wachague lugha ya kusema wanapotaka kushauri au kuzingumza jambo kwa Rais.

“Kikubwa lazima tutambue kila kabila na utamaduni wake.Lugha ambazo unaweza kuzitumia kumwambia  Mzaramo au Mkwere anaweza kucheka lakini lugha hiyo hiyo ukiitumia kwa Mkurya atakukata panga.

“Lugha ambazo unataka kumwambia Rais wa Serikali ya Awamu Tano lazima ziwe na staha kwani kinyume na hapo anaweza kukupa jibu ambalo litakukwaza.Tukubali kuwa mila na desturi zinatofautina sana,”amesema Shibuda.

Akifafanua katika hilo Shibuda ametoa mifano kuwa hata unapotaka kwenda kuoa ukienda kutoa posa Bukoba watakwambia nenda na mkungu wa ndizi, ukienda Tanga watakwambia nenda na kuku wa kitoweo na ukienda Usukumani utaambiwa uswage Ng’ombe.

“Vivyo hivyo hata unapotaka kumshauri Rais lazima uzingatie mila na desturi.Nimeona hili niwaambie kwani kuna changamoto ya matumizi ya lugha miongoni mwetu,”amesema Shibuda.

Kuhusu hofu ya kufutwa vyama vingi ambayo wanasiasa wengi wameionesha kwenye mkutano huo,Shibuda amewahakikishia kuwa Rais hawezi kuvifuta wala kudhoofisha demokrasia bali ataimarisha.

Amesema kuna mambo mengi yanayoendelea ndani ya vyama vya siasa na kwamba wanaendelea na mazungumzo na mwisho watakapomaliza wataeleza umma kupitia vyombo vya habari.

Wakati huo huo wanasiasa wa vyama vya siasa nchini wameonesha kukerwa na tabia ya wanasiasa wanaohama vyama kila kukicha na kusababisha gharama kubwa za kurudia uchaguzi.

Wanasiasa hao wamejadili eneo hilo kwa kina na kufikia muafaka iko haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu vyama vya siasa pamoja na chaguzi mbalimbali.

Awali Katibu Mkuu wa Jukwaa la Katiba Tanzania(Jukata) Deus Kibamba amesema alitoa pendekezo linalosema iwe ruksa kuhama chama cha siasa bila kupoteza nafasi ya kuchaguliwa na bila kuhitajika uchaguzi mpya.

Kibamba amesema kutokana na wimbi la wabunge na madiwani kuhama vyama kwasababu mbalimbali na malalamiko ya Watanzania kuhusu gharama kubwa zinatumika katika chaguzi ndogo kutokana na wanasiasa kuhama vyama.

“Na kwa kuwa Taifa linaingia katika kipindi cha uchaguzi muda si mrefu ujao.Jukata tumetafakari na kuona ipo haja ya kuruhusu mfumo wa wanasiasa kuhama vyama pasipo kupoteza nafasi zao za kuchaguliwa.Hii italiokolea taifa fedha nyingi kiasi cha kuendeleza nchi yetu kiuchumi na maendeleo,”amesema Kibamba.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )