Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Monday, August 27, 2018

Polisi Wavunja Mkutano wa Vijana Dar Na Waandishi wa Habari........Uliitishwa Kwa Ajili ya Kujadili Demokrasia na Haki za Binadamu

Jeshi la Polisi jana lilivunja mkutano ulioandaliwa na taasisi za vijana kuzungumzia mwenendo mbovu wa haki za binadamu na uvunjwahji wa haki za msingi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mkutano huo uliotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Landmark, Ubungo kuanzia saa tano asubuhi jana, ulikwama kuendelea baada ya kuvamiwa na polisi huku waandaaji wakitimua mbio kwa hofu ya kutiwa nguvuni.

Wakati waandaaji wa mkutano uliopangwa kuanza saa tano asubuhi  jana Agosti 26, 2018 katika Hoteli ya Landmark, Ubungo jijini Dar es Salaam wakiendelea na maandalizi, ghafla aliingia ofisa mmoja wa polisi aliyekuwa amevalia sareza jeshi hilo na kujitambulisha kwa mlinzi kwamba naye ni mshiriki.

Baada ya kupewa maelezo, ofisa huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana alimweleza mlinzi huyo kuwa hawezi kuingia kutokana na sare zake za kazi na kuita askari wengine waliovalia kiraia ambapo alitoka nje na baada ya muda waliingia askari polisi waliokuwa na silaha za moto kwenye ukumbi wa mkutano.

Hatua hiyo ilizua taharuki miongoni mwa wanahabari na waandaaji wa mkutano huo, baada ya kubaini kuzingirwa na askari kanzu waliovaa kiraia huku askari wenye silaha wakizingira pia eneo hilo na hivyo kuwalazimu waandaaji na wanahabari kila mmoja kuanza kutawanyika ki vyake.

Akizungumzia tukio hilo, Mratibu wa Uhusiano kwa Umma wa Taasisi ya Tanzania Sahrawi Solidarity Committee  (TASSC), Noel Shao alisema walilazimika kusitisha kutoa tamko lao ukumbini hapo baada ya kuhofia usalama kutokana na kuzingirwa na polisi.

“Polisi wenye sare na silaha na askari kanzu wakiwa ndani ya gari zisizo pungua nne za polisi ziliendelea kupiga kambi kwenye Hoteli ya Land Mark kwa zaidi ya saa moja kuhakikisha hatutoi tamko. 

"Hata hivyo, tutaendelea kuwasiliana na umma kupitia njia nyingine za mawasiliano ili kupaza sauti zetu dhidi ya ukandamizwaji wa demokrasia na haki za binadamu,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Muliro alipotafutwa alisema uwapo wa polisi eneo la hoteli hiyo ni sehemu ya doria ya kawaida.

“Hivi polisi alipo watu wakimbie? Ebu wahoji hao kwa nini walikimbia. Sisi tutaendelea kuwapo na hata sasa ukienda mahotelini utaona polisi, je watu wanakimbia?” alihoji Muliro na kuongeza:

“Wewe si unaona polisi mitaani je watu wanakimbia?  Waulizeni wao kwa nini walikimbia.”

Hata hivyo, muda mfupi baadae, waandaaji hao walitoa taarifa yao  ikiwa imeorozesha waandaaji kuwa ni Taasisi za Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG), Kamati ya Mshikamano Kati ya Tanzania na Sahara Magharibi (TASSC) na Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP).

Kwa pamoja, mitandao hiyo kupitia kwa mratibu wao, Shao walieleza kuwa wanaharakati wa haki za binadamu, asasi za kiraia na wananchi karibu nchi zote za Afrika Mashariki  wamekuwa wakishughulikiwa ili kuhakikisha baadhi ya tawala  zinatawala bila kikwazo.

Alisema katika kufanikisha hilo, wapinzani wa serikali wanashambuliwa, wanauawa, kubambikiwa kesi, kuozea jela bila hatia, kufilisiwa au kuzuiwa nje ya nchi kwa fimbo ya uraia suala ambalo halipaswi kukaliwa kimya.

Alisema wamefadhaishwa na kushamiri kwa vitendo vya ukandamizwaji wa  haki za binadamu, kusiginwa kwa misingi ya kidemokrasia na utawala bora na kuchipua kwa siasa za mkono wa chuma chini ya mtu mmoja badala ya utawala wa taasisi za umma na vyombo vya uwakilishi wa watu.

Shao alisema kwa Uganda, wameshtushwa na hatua ya hivi karibuni ya Serikali ya Rais Museveni kumkamata, kumshikilia kwenye korokoroni ya kijeshi, kumtesa na kumfungulia mashtaka bandia ya kukutwa na silaha Mwanamuziki na Mbunge wa Jimbo la Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulani, maarufu kwa jina la Bobi Wine.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

taboola apo chini
....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )