Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Wednesday, August 8, 2018

Serikali: Nane Nane Isingoje Mwezi Wa Nane

Na. Atley Kuni- Simiyu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo, amewataka Maafisa Kilimo kuhakikisha kuwa wanaendelea kutoa utaalamu wa kilimo katika mabanda ya Nanenane hata baada ya maonesho hayo kukamilika ili wananchi waweze kufaidi utaalamu wao

Aliongeza kuwa ipo haja kwa kila kanda kunapofanyikia maonesho ya Nanenane kuandaa wataalamu wa kilimo ambao watakuwa wakiendelea kutoa huduma hizo hata baada ya maonesho hayo kumalizika

Waziri Jafo alitoa kauli hiyo jana kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu, kabla ya kuzindua mwongozo wa namna ya kuandaa mipango ya kilimo ya wilaya (District Agricultural Development Plans Guideline- DADPs Guideline).

Alisema kuwa mwaka jana akiwa jijini Dodoma aliagiza kuwa wataalamu wa kilimo hawana budi kuwa na watumishi wa kudumu katika vibanda vya maonesho ili waweze kutoa utaalamu wao kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo.

“Wakulima wetu hawapaswi kungoja msimu wa Nane Nane ndio waje kujifunza mbinu na maarifa ya ukulima bora ambao utakuwa na manufaa kwao bali inatakiwa kila mkulima anapotaka kujifunza ajue lipo eneo ambapo anaweza kwenda na kupata ushauri nasaha juu ya jambo linalo mtatiza katika Mifugo, Kilimo au Uvuvi” alisema Jafo.

Mhe. Jafo alisema asilimia 65 ya malighafi za viwanda hutokana na mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi hivyo suala la wananchi wanaofanya shughuli hizo kuwa endelevu halina budi kuzingatiwa na kupewa kipaumbele.

“Tunapoendelea na Kampeni ya Kiwanda changu mkoa wangu ambapo tumeonekana kufanya vizuri katika robo ya kwanza na kufikia asilimia 49 ya malengo ya kuwa na viwanda 100 kwa kila mkoa lazima tujidhatiti katika kutoa utaalam wa kutosha kwa wakulima wetu,” alisema Jafo.

Mbali na uzinduzi wa mwongozo wa kilimo wa wilaya, Mhe. Jafo pia alikagua na kujionea shughuli mbali mbali zinazoendelea katika kanda hiyo inayounganisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga na kujionea Vipando kutoka Halmashuri za Mikoa hiyo, Mabanda ya Biashara sambamba na kujionea shughuli ndogo ndogo za wajasiriamali zikiwepo shughuli za usindikaji.

Waziri huyo mwenye dhamana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa alifanikiwa pia kutembelea Banda la Wizara yake pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara yake kisha kuwapongeza kwa namna wanavyo toa huduma kwa wananchi.

“Niwape pongezi kwa kweli kwa kazi kubwa mnayofanya, wingi wa watu wanaowafikia kutaka ufafanuzi wa masuala mtambuka ni ishara kwamba wananufaika na elimu mnayowapa hivyo endeleeni kutoa huduma,” alisema Waziri Jafo.

Mapema kabla ya kuzindua mwongozo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Kisekta kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa bwana Leo Martin Mavika alieleza kuwa mwongozo huo unalenga kuelezea hatua kwa hatua namna ya kushirikisha wananchi na wadau mbalimbali katika kuandaa mpango wa maendeleo ya kilimo wa kijiji.

Aliongeza kuwa mwongozo huo pia unalenga kuunganisha mipango ya vijiji katika kata na hatimaye kupata mpango wa  wilaya.

Bwana Mavika alisema kuwa mwongozo huo utatumika katika kuandaa mipango ya kilimo kuanzia mwaka wa fedha 2019/20. Kabla ya kufikia kipindi hicho timu ya uwezeshaji wa taifa itatoa mafunzo ya namna ya kutumia mwongozo huo kwa mikoa na halmashauri zote Tanzania

Maonesho ya Nane Nane ya 2018 yanafanyika mkoani Simiyu na yanabebwa na kaulimbiu “Wekeza katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Maendeleo ya Viwanda. 
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )