Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Sunday, August 12, 2018

TIB Kushirikiana Na Taasisi Nyingine Ili Kuinua Sekta Ya Kilimo Nchini

MKURUGENZI wa Benki ya Rasilimali(TIB) Bw. Charles Singili amesema kuwa watashirikiana na taasisi nyingine za fedha ili kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za Rais Dk.John Magufuli katika kuinua sekta ya kilimo nchini.

Ametoa kauli hiyo jana wilayani Kibaha mkoani Pwani wakati wa tukio la kukabidhiwa kwa matrekta 10 yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa Chuo cha Kilimo(SUA) cha mkoani Morogoro ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais kwa chuo hicho.

Alisema TIB inatambua na kuthamini jitihada za Rais kwenye kuinua kilimo nchini na wao wanalo jukumu la kuhakikisha malengo na mikakati ya Serikali inafanikiwa.

Alifafanua kwamba TIB wanashukuru kwa kujumuishwa kwenye tukio hilo la kukabidhiwa matrekta hayo kwa SUA hasa kwa kuzingatia nao ni wadau muhimu katika eneo la kilimo.

Aliongeza kuwa Serikali ilifanya uamuzi wa kuanzisha dirisha la kilimo mwaka 2009 ikiwa ni maandalizi ya kuanzisha benki ya kilimo na ilitenga Sh.bilioni 42 ambayo nia yake ilikuwa kuanza kuchochea ukuzaji wa kilimo.

Alifafanua baada ya kuanzishwa benki hiyo moja ya eneo ambalo walijikita ni kwenye zao la pamba na kwamba  wanao ujuzi wa kutosha kwenye eneo la ukopeshaji hasa katika zana za kilimo.

“Kutokana na uwezo huo tulifanikiwa  kutoa mkopo katika eneo hilo na zana za kilimo ambapo tumekopesha matrekta 249.

“Na bahati nzuri chini ya Wizara yako (Wizara wa Fedha)  ipo na Benki Kuu(BoT) na kuna sheria inayotuongoza katika kutekeleza vema majukumu yetu,”alisema Singili.

Alisema kutokana na uwepo wa sheria hiyo wamekuwa na utaratibu mzuri wa utoaji mkopo wa zana za kilimo ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea baadhi ya changamoto.

 Singili alisema changamoto ya kwanza ni ile ambayo ilikuwa inatokana na kukosekana kwa mzunguko unaohitajika ambao ni uwepo wa kiwanda cha matrekta na hivyo kubaki na mzunguko benki ambayo ni mkopeshaji pamoja na mkopaji.

Alisema juhudi za Serikali za kuhakikisha kuna kuwa na kiwanda hicho kumekamilisha mzunguko unaotakiwa kwani sasa kutakuwa na mwenye kiwanda, benki na mkopeshwaji.

“Unapokuwa huna mwenye kiwanda ambaye ndiye mtengenezaji wa zana za kilimo maana yake inapoharibika hasara inabaki kwa anayetoa mkopo na aliyekopeshwa.

“Kwa sasa hata trekta linapoharibika inakuwa rahisi kwani aliyetengeneza yupo hivyo hakutakuwa na changamoto ambayo ilikuwa awali,”alisema Singili.

Alitaja changamoto nyingine iliyokuwepo ni ubora wa zana za kilimo ambayo nayo ilisababisha chombo kinapoharibika basi mkopaji anashindwa kulipa mkopo na matokeo yake benki inakuwa kwenye wakati mgumu ambapo kwa sasa hilo nalo limepata ufumbuzi wake.

Alitumia nafasi hiyo kueleza kwamba uwepo wa matrekta hayo usiwe tu kwa ajili ya kutumika  kulima na kuvuta bali sasa yatumike katika kuongeza thamani ya mazao ya mkulima ili naye anufaike.

Alifafanua kwamba injini ya trekta inapozunguka inaweza kufanya kazi za zaidi ya moja kwani mashine hizo zikiungwanishwa na mashine nyingine inaweza kutumika kwa kufanya kazi nyingine.

“Ni wakati sasa wa kutazama na kuhakikisha  injini ya tekra inatumika kwa  kufanya mambo mengine kwa lengo la kumuwezesha mkulima kuongeza thamani ya mazao yake,”alisema Singili.

Alisisitiza ameona kuna trekta zenye puli zaidi ya moja na hivyo badala ya kulima na kuvuta trekta likiwaka linaweza kutumika kwa ajili ya shughuli nyingine.

Alitumia nafasi hiyo kumueleza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James kwamba wapo tayari kushirikiana na taasisi nyingine kufanikisha malengo hayo.

Alisema mahitaji ya nchi ni matrekta milioni 2 na unapoangalia gharama yake ni kubwa  hivyo ili kufanikisha inahitaji nguvu ya pamoja.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )