Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Wednesday, September 26, 2018

Kiswahili Kuwa Lugha Kuu Ya Mawasiliano Barani Afrika

adv1
Na Fatma Salum-MAELEZO
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amebainisha kuwa lugha ya Kiswahili inatarajiwa kuwa lugha kuu ya mawasiliano katika bara la Afrika ifikapo mwaka 2063.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Kampeni Ya Uzalendo na Utaifa kwa mwaka 2018 yanayotarajiwa kufanyika Desemba 8 Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Pombe Magufuli.

Alisema kuwa kampeni hiyo kwa mwaka huu imejikita katika kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ambayo ni kielelezo kikubwa cha utashi na uhai wa taifa la Tanzania na inakua kwa kasi sana barani Afrika na duniani kote kwa ujumla.

“Sasa hivi Kiswahili ni lugha ya kumi kati ya lugha elfu 6 zinazoongelewa na watu wengi duniani na kwa mujibu wa Tafiti za Umoja wa Afrika zinaonesha kuwa ifikapo mwaka 2063 Kiswahili kitakuwa lugha kuu ya mawasiliano katika bara la Afrika na utambulisho wa mtu mweusi duniani,” alisema Mwakyembe.

Alieleza kuwa dunia yote inatambua kwamba Tanzania ndio chimbuko la lugha adhimu ya Kiswahili hivyo watanzania wanapaswa kujivunia lugha hiyo na kuitangaza kwa kuwa ni sehemu ya utamaduni wa taifa na msingi wa uzalendo na utaifa.

Waziri Mwakyembe alibainisha kuwa kampeni hiyo mwaka huu imejikita katika kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ili kuwasisitiza watanzania kuthamini lugha yao na utamaduni wao na kurejea kwenye misingi ya maadili ya taifa lao.

Alisema kuwa sasahivi kuna changamoto kubwa ya mmomonyoko wa maadili inayosababishwa na baadhi ya watu hasa vijana kuiga tamaduni za nje kutokana na utandawazi hivyo kupelekea kudharau utamaduni wao ikiwemo lugha ya Kiswahili jambo ambalo lisipochukuliwa hatua madhubuti litaleta athari kwa jamii.

Pia Waziri Mwakyembe alitoa pongezi kwa Rais John Pombe Magufuli kwa mchango wake mkubwa anaoonesha katika kutumia, kukuza na kuitangaza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi hivyo amekuwa ni mfano wa kuigwa.

Aidha alitoa rai kwa watanzania wote na wadau mbalimbali kuunga mkono kampeni hiyo kwa hali na mali ili Tanzania iweze kufanikiwa kulinda misingi ya utamaduni na utaifa hususan lugha ya Kiswahili.

Kampeni ya Uzalendo na Utaifa ilianza rasmi mwaka jana 2017 na itakuwa ikiadhimishwa kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu yake ni ‘Kiswahili Uhai Wetu, Utashi Wetu’. 
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )