Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Wednesday, September 26, 2018

Rufaa ya Vigogo CHADEMA Yaibua Mvutano Mahakamani

Rufaa ya viongozi wa Chadema iko njia panda baada ya Mahakama ya Rufani kuhoji uhalali wa taarifa ya kusudio la kukata rufaa hiyo ambayo ndiyo msingi wa rufaa yenyewe.

Mahakama hiyo imehoji uhalali wa taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa leo wakati rufaa hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji baada ya kubaini upungufu kwa kutokueleza asili ya amri au uamuzi ambao wanaukatia rufaa.

Katika rufaa hiyo viongozi hao wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe wanapinga uamuzi wa Mahakama Kuu.

Rufaa hiyo ni mwendelezo kutokana na kesi ya msingi ya jinai inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo wanapinga uamuzi na amri mbalimbali ambazo mahakama hiyo imekuwa ikizitoa.

Awali, walifungua maombi ya mapitio Mahakama Kuu wakiiomba Mahakama hiyo iitishe jalada la mwenendo wa kesi ya msingi na kuuchunguza pamoja na amri zake ili kujiridhisha na usahihi na uhalali wa mwenendo na amri hizo.

Hata hivyo, mjibu maombi (upande wa mashtaka) kupitia kwa jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi uliweka pingamizi ukiomba Mahakama hiyo iyatupilie mbali kwa madai ni batili kutokana na kukiuka sheria ya Mahakama za hakimu mkazi.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Rehema Sameji aliyesikiliza maombi hayo ilikubaliana na hoja za pingamizi za Jamhuri na ikaitupilia mbali maombi hayo ndipo wakakata rufaa wakaenda Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo.

Kabla ya kuanza usikilizwaji huo, Jaji Mbarouk aliwataka mawakili wa pande zote kutoa maoni yao iwapo taarifa ya kusudio la kukata rufaa imekidhi matakwa ya kanuni za Mahakama hiyo.

Jaji Mbarouk alisema kanuni za Mahakama hiyo za uendeshaji wa mashauri ya jinai kanuni ya 68 (2) zinaelekeza taarifa ya kusudio la kukata rufaa lazima iainishe asili ya uamuzi au amri ambayo inakatiwa rufaa.

Wakili Peter Kibatala wa wakata rufaa licha ya kukiri kanuni hiyo inaelekeza taarifa ya kusudio la kukata rufaa kuonyesha asili ya uamuzi unaokatiwa rufaa, lakini alisema hata hivyo kutokuonesha hivyo hakuna athari.

Alisema lengo la taarifa hiyo ni kutoa ujumbe tu kuwa kuna jambo linalolalamikiwa na kwamba zipo kesi nyingi za rejea, huku akisema jambo hilo lingekuwa na athari kama wangekuwa wanapinga sehemu tu ya uamuzi lakini wao wanapinga uamuzi wote wa Mahakama Kuu.

Wakili Mtobesya kwa upande wake alisema taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa iko sahihi na kwamba hapakuwa na haja ya kubainisha wanachokikatia rufaa kwani wanakata rufaa dhidi ya uamuzi wote na si sehemu tu ya uamuzi.

Wakili wa Serikali Kadushi akisaidiana na mawakili wenzake, Dk Zainabu Mango, Wankyo Simon na Jacquiline Nyantori walidai kwa mujibu wa kanuni hiyo ni sharti la msingi kuainisha asili ya uamuzi au amri inayokatiwa rufaa.

Alidai kutokufanya hivyo taarifa hiyo inakuwa batili na inapaswa kutupiliwa mbali na kwa kuwa rufaa inatokana na  taarifa ya kusudio la kukata rufaa basi nayo inakufa moja kwa moja.

Naye Wakili Kadushi alisisitiza kuwa kwa kua taarifa ya kusudio la rufaa haijakidhi matakwa hayo inakosa uhalali wa kisheria kuanzisha rufaa hiyo na akaiomba Mahakama iitupilie mbali, huku akiongeza kuwa rufaa hiyo haiwezi kusimama.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote iliahirisha shauri hilo hadi tarehe itakayopangwa ambayo watajulishwa kwa ajili ya uamuzi.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu, Dk Vicent Mashinji, manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Pia wamo Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 ambayo ni kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali yanayowakabili wote, huku Mbowe, Msigwa Mdee na Heche kila mmoja peke yake akikabiliwa na mashataka zaidi.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16 katika barabara ya Kawawa, Mkwajuni, Kinondoni, siku wakihitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni na kusababisha vurugu zilizosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )