Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Saturday, October 6, 2018

Rais Magufuli Apokea Taarifa Ya Udhibiti Mapato Ya Serikali

Rais  John Magufuli amepokea taarifa ya maendeleo ya kazi ya udhibiti wa mapato ya serikali kutoka kwa timu ya wataalamu wanaotengeneza na kusimamia mifumo ya mapato ya serikali, wakaguzi na wataalamu wa bajeti. 

Alipokea taarifa hiyo jana ikulu kutoka timu inayoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James iliwasilisha taarifa ya uanzishwaji wa mifumo katika taasisi za umma 304 nchini, ongezeko la mapato baada ya kuwekwa kwa mifumo hiyo, ukaguzi wa ndani na masuala ya bajeti.

Katibu Mkuu Doto James alimueleza Rais Magufuli kuwa katika kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi 2017/2018 timu hiyo imefanikisha kuokoa zaidi ya Sh trilioni 3.2 zikiwamo Sh trilioni 2.2 zilizookolewa kutoka kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii baada ya kufanya uhakiki wa madeni ya serikali, kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti feki. 

Doto alibainisha kuwa timu hiyo pia imefanikiwa kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za serikali baada ya kuziunganisha taasisi 304 katika mfumo unaodhibitiwa moja kwa moja na Wizara ya Fedha na Mipango.

Taasisi hizo ni pamoja na zinazokusanya maduhuli ya serikali kama vile Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Idara ya Ardhi, Wakala wa Vipimo, Hifadhi za Taifa (Tanapa), Wakala wa Misitu, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Hifadhi ya Ngorongoro na Wizara ya Ardhi, na kuondoa mawakala wa kulipa mishahara ya watumishi. 

Rais Magufuli aliwapongeza wataalamu hao kwa kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya na alimuagiza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi kuhakikisha taasisi zote za serikali zinazopaswa kuunganishwa na mifumo hiyo ya udhibiti zinaunganishwa haraka iwezekanavyo, vinginevyo awachukulie hatua viongozi ambao hawatatekeleza agizo hilo.

“Nimefurahi sana kwamba sasa vijana wetu mmeweza kutengeneza mifumo yetu sisi wenyewe kwa ajili ya kudhibiti mapato ya serikali, nawapongeza sana, mnafanya kazi kubwa ya kujenga nchi yetu, mmeonesha uzalendo wa hali ya juu, nawahakikisha nipo na nyinyi na endeleeni kuchapa kazi.

 “Mmeaniambia kuwa mpaka sasa mmeunganisha mifumo ya kudhibiti mapato kwa taasisi 304 na bado kuna taasisi nyingi bado hazijaunganishwa, naagiza taasisi zote za serikali zitumie mifumo mnayoitengeneza na ambayo inadhibitiwa na sisi wenyewe.

“Nafahamu mmeokoa fedha nyingi sana ambazo zilikuwa zinapotea, hatuwezi kuendelea kuachia fedha ziendelee kupotea,” alisisitiza Rais Magufuli. 

Aliongeza kuwa fedha ambazo zimepatikana baada ya udhibiti wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato ndizo zimesaidia kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ajili ya wananchi ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya 208 katika nchi nzima. 

Mingine ni ujenzi wa hospitali mpya 67, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (SGR), madaraja makubwa na madogo, barabara, kusambaza umeme, maji na mingine mingi iliyotekelezwa katika kipindi kifupi cha tangu serikali iingie madarakani.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )