Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Saturday, October 27, 2018

Waziri Lukuvi Alitaka Shirika La NDC Kulipa Kodi Ya Ardhi Kufikia Desemba 2018

Na Munir Shemweta, WANMM Kilimanjaro
Waziri wa Ardhi nyumba na maendeleo ya Makazi Mhe William Lukuvi amelitaka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kulipa kodi ya ardhi katika eneo inalolimiliki la Viwanda lililopo Weruweru wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro kabla ya desemba mwaka huu.

Aidha, Mhe Lukuvi amewataka wote waliokuwa katika eneo hilo bila ya hati wala offer kutoendelea kuwepo eneo hilo kwa kuwa hawana uhalali wa kumiliki maeneo katika eneo la Weruweru.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ameelekeza ufanyike ukaguzi kwa kila kiwanja katika eneo la viwanda la Weruweru lenye ukubwa wa ekari 1103 kwa lengo la kuwabaini viwanja vyote visivyoendelezwa na  watakaobainika watanyanganywa maeneo hayo kwa mujibu wa sheria.

Mhe. Lukuvi alitoa kauli hiyo jana alipotembelea eneo la viwanda la Weruweru wakati wa Ziara yake ya  kushughulikia migogoro ya ardhi katika wilaya za Hai, Moshi na Same mkoa wa Kilimanjaro.

NDC inamiliki eneo la viwanda lenye ukubwa wa ekari 626 kikiwemo kiwanda cha kutengeneza mashine mbalimbali kama vile za kusaga, kukoboa na kuranda mbao cha Kilimanjaro Machine Tools Manufacturing Co Ltd ambapo kati ya ekari hizo 80 tayari zina hati huku ekari 546 zikiwa na offer.

Lukuvi ameshangazwa na NDC kushindwa kulipa kodi ya ardhi katika kipindi chote wanachomiliki eneo hilo huku wakiwakodisha wananchi kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo na kueleza kuwa Shirika hilo la Maendeleo la Taifa litakapo lipa kodi yote ya ardhi litapatiwa hati ya umiliki katika eneo lenye offer.

“Kosa lenu NDC mnakodisha watu masikini halafu ninyi hamlipi kodi ya ardhi sasa mnatakiwa kulipa kodi ya ardhi tangu mlipoanza kumilikishwa eneo hilo kufikia desemba mwaka huu 2018” alisema Lukuvi

Kwa mujibu wa Lukuvi katika eneo la viwanda la Weruweru kuna watu  wameshikilia maeneo kwa muda mrefu tangu mwaka 1985 bila kuyaendeleza huku wengine wakibadilisha matumizi hivyo aliagiza wote wapewe Ilani ya ubatilisho na ikibidi serikali itafuta miliki zao na kuyagawa maeneo hayo kwa watu wengine ili wajenge viwanda.

Meneja wa kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools Manufacturing Co Ltd Andreano Nyaluke  alijitetea kwa kusema kushindwa kulipa kodi  ya ardhi katika muda wote wa umiliki kunatokana na uwezo mdogo wa kiwanda  ingawa amesema jitihada zinafanyika ikiwemo kutafuta mkopo kwa ajili ya kuendeleza kiwanda.

Kauli hiyo haikumfurahisha waziri Lukuvi hasa baada ya kubaini NDC kukodisha sehemu ya eneo hilo kwa wananchi kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo ambapo wastani wa watu 50 hadi 300 hukodishwa katika kila msimu wa kilimo kwa gharama ya shilingi laki moja kwa ekari moja.

Wakati huo huo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe William Lukuvi ametaka kufanyika tathmini katika shamba la Fofo wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro na baadaye serikali itafanya maamuzi kulingana na uamuzi wa Mahakama.

Hatua hiyo ya Lukuvi inafuatia mgogoro uliopo katika shamba hilo ambapo kundi la watu 48 linamiliki shamba  hilo na kuacha wananchi wengine wakihangaika huku kiasi cha shilingi milioni 2.6 zikiwa zimelipwa kwa wahusika kama gharama za fidia .
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

taboola apo chini
Loading...
....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )