Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Saturday, November 24, 2018

Serikali Yafafanua Utolewaji Wa Vibali Kwa Ajili Ya Uchimbaji Visima Nchini

Serikali imewatoa hofu wananchi kuhusu utaratibu ulioanzishwa kwa wenye visima kuanza kuvilipia na kueleza kuwa haina nia ya kuwakomoa wananchi bali sheria inawataka kufanya hivyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa, Kitilia Mkumbo, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa masuala ya maji pamoja na visima.

Prof. Mkumbo alikuwa anatoa ufafanuzi kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliyetaka kujua ni visima gani hasa ambavyo vinalengwa na serikali.

"Mkoa wangu una visima vingi moja wapo ni hivi ambavyo wananchi wangu wamejichimbia maji nyumbani mita 12 na wengine kwa sababu hatujawafikishia maji asilimia 100 waliona wana uwezo wa kuchimba visima na kuwasambazia wenzao," alisema na kuongeza:

"Sasa juzi nimesikia kauli ambayo kidogo imeleta taharuki na kuna visima zaidi ya 3,000 naomba na hili utupe kauli yako na Sheria inasema nini maana wanaona kama serikali inawatisha," alisema Makonda.

Mkumbo alisema visima hivyo vimegawanywa katika makundi matatu, la kwanza ni la visima ambavyo havihitaji kibali wala mhusika halipii chochote, la pili vinavyohitaji kibali na kulipa wakati cha tatu ni kile cha kiwango cha kufanya biashara kama viwanda.

Alisema wenye viwanda wote wanafahamu taratibu za kumiliki visima, namna ya kutumia maji na wakulima wakubwa kwa kuwa kila mwaka wanaomba vibali lakini changamoto inakuwa katika kundi la kwanza na pili.

Alisema kwa kundi la kwanza kwa mujibu wa sheria, kama mtu anachimba maji nyumbani chini ya mita 15 kwa ajili ya kwa matumizi ya nyumbani na hajaweka miundombinu yoyote, hahitaji kibali wala kulipia.

"Lakini kama utatengeneza mita 15 au zaidi, ukaweka miundombinu kama mashine za kusukuma maji, hapa utahitaji kibali na ukifuata maji zaidi ya mita 15 utalipia ada fulani kutokana na kiwango cha maji. Hizi ndizo taratibu za msingi," alisema.

Mkumbo alisema suala hilo limewekwa hivyo kwa makusudi ili mhusika atumie maji katika hali ambayo haitaathiri watu wengine, atumie katika hali isiyoathiri mazingira na atumie maji hayo katika hali ambayo itawezesha kutumika na vizazi vijavyo.

"Lengo la kufanya hivyo si kumkomoa mwananchi hata kidogo. Serikali inatambua ni lazima upate maji na imeweka utaratibu wa kawaida wa kurahisisha kupata maji," alisema.

Katibu Mkuu alisema kwa bahati mbaya sheria hizo zilikuwa hazifuatwi na kwa sasa wameanza kufuatilia visima ingawa kumekuwa na changamoto.

Alisema wanatoa elimu kwa wananchi ili waelewe hizo taratibu na kuzizingatia na anaamini kwamba watanzania ni watu wanaofuata taratibu baada ya kuzielewa sheria.

"Katika mchakato huu wa kutekeleza sheria hiyo kama kutajitokeza changamoto za kisheria ndio maana kuna Bunge, wananchi watatoa malalamiko yao na Bunge letu watalichukua na kulifanyia kazi lakini kwa sasa utaratibu ndio huo," alisema.

Aidha, Mkumbo alisema maji ni rasilima ya nchi hivyo mtu binafsi hawezi kusema anamiliki maji yake.

Alisema kwa sababu maji ni rasilimia ya taifa ni lazima kuwepo na utaratibu wa kuipata na Rais ndiye aliyekabidhiwa kuisimamia.

"Wapo wananchi na wafanyabiashara wamechimba visima kwa bahati mbaya bado hatujavitambua vyote kwa sababu hatujapata taarifa kutoka kwa wananchi. Tumeagiza maofisa wetu katika mikoa yote kuanza kufanya kazi ya kuvitambua," alisema

Mkumbo alisema Sheria ya mwaka 2009 na 2011 ya rasilimali za maji imeweka taratibu zake kuhusu namna wananchi wanavyoweza kujishughulisha katika kupata maji.

Aidha, alisema wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji na ifikapo 2020 wana uhakika wa kupunguza tatizo la maji kwa asilimia kubwa.

Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

taboola apo chini
....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )