Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Sunday, November 11, 2018

Serikali Yakitwaa Kiwanda Cha Kuchakata Korosho Lindi (Buko)

adv1
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) yenye dhamana ya kusimamia mali za Serikali kwa sehemu ambazo Serikali imefanya uwekezaji, imekitwaa Kiwanda cha Kuchakata Korosho Lindi maarufu kama BUKO kilichojengwa mwaka 1978 na kufanya uzalishaji kwa kipindi cha miaka nane tu kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 10,000 kwa mwaka huku lengo likiwa ni kufikia tani 60,000 kwa mwaka.


Akizungumza katika kikao cha awali na Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi kuelezea utaratibu mzima ulivyokua mpaka Serikali kufikia uamuzi huo kabla ya zoezi la utwaaji wa kiwanda uliofanyika kiwandani eneo la Viwanda la Jamhuri pembezoni mwa barabara iendayo Mtwara, Kaimu Msajili wa Hazina (TR) Ndg.Peter Gwagilo, alisema hii ni sehemu tu ya utekelezaji wa kasi na Sera ya urejeshaji viwanda vilivyobinafsishwa au kuuzwa na Serikali miaka ya nyuma na kubainika kutofanya kazi kwa tija kama ilivyotarajiwa kwa mujibu wa mikataba iliyoingiwa na wawekezaji husika hivyo viwanda kufa au kufanya kazi kwa kusuasua kutokana na uwekezaji hafifu tofauti na makubaliano.

Kaimu Msajili wa Hazina akitanabaisha nia njema ya Serikali katika urejeshaji wa viwanda vya mtindo huu amesema utwaaji hufanyika baada ya kujiridhisha kutokana na zoezi linalofanyika kila baada ya miezi mitatu la ufuatiliaji na tathmini kuangalia utekelezaji wa mikataba ya uwekezaji iliyoingiwa lengo mahususi likiwa ni kujiridhisha utekelezaji wa mikataba ambayo Serikali imeingia na mwekezaji.

Ndg.Gwagilo amewasihi wawekezaji walioingia mikataba ya uwekezaji na Serikali kutekeleza kama mikataba inavyoainisha kwani zoezi la urejeshaji viwanda hivi bado ni endelevu na Serikali inaendelea na taratibu zinazotakiwa katika kupata wawekezaji wengine wenye uwezo, tija na nia madhubuti ya kuwekeza kwenye viwanda hivyo na tayari utwaaji huu umeshafanyika kwenye mikoa kadhaa ikiwemo ya Kilimanjaro (Kiwanda cha kutengeneza madawa ya mimea Moshi na Kiwanda cha Kukoboa Mpunga Kilimanjaro), Tanga (Kiwanda cha Magogo ya Mbao) na sehemu nyingine kama Kiwanda cha Maziwa UTEGI mkoani Mara, ambapo kwa awamu hii jumla ya viwanda 12 kikiwemo hiki cha Korosho Lindi kilichokwishatwaliwa vinatarajiwa kurejeshwa Serikalini baada ya kujiridhisha vya kutosha kuwa mwekezaji ameshindwa kuwekeza kulingana na mkataba.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Lindi Ndg.Godfrey Zambi akipokea ujumbe wa wataalamu Wilayani Kilwa kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina na Ofisi ya Rais tayari kwa zoezi hilo alisema, “Naishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina kufanya maamuzi haya sahihi kwani kiwanda hiki hakijawahi kufanya uzalishaji wenye tija kwa Taifa kama tulivyotarajia na hii inatokana na madhaifu yaliyobainika katika zoezi zima la ubinafsishaji lililofanyika awali miaka ya nyuma ambapo kwa sehemu kubwa mikataba hii ndiyo imeigharimu Serikali yetu.”

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Lindi Ndg.Shaibu Issa Ndemanga ameitaka Ofisi ya Msajili wa Hazina kutokata tamaa kutokana na changamoto mbalimbali inazokumbana nazo katika mazoezi haya ya ufuatiliaji, kufanya tathmini na utwaaji pale inapolazimu kwani Serikali ni moja na hivyo ni vema kuwa na utaratibu wa mawasiliano ya moja kwa moja na Msajili wa Hazina katika kuyazungumzia haya kuepusha wazungumzaji wengi kwa jambo moja jambo linaloweza kuleta upotoshaji wa taarifa.

Hali kadhalika nae Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Ndg.Rehema Madenge ameishauri Serikali kufanya maamuzi ya kukiendesha yenyewe kiwanda hiki kutokana na uwekezaji na uendeshaji duni kabisa wa mwekezaji katika kiwanda hiki uliopelekea kutokuwepo kwa uzalishaji na badala yake kutumia majengo kama maghala ya kuhifadhia mazao na vitu mbalimbali kwa kuyakodisha kitu ambacho ni tofauti kabisa na lengo la Serikali katika ubinafsishaji na uuzaji wake kwa wawekezaji.

Pamoja na hilo Ndg.Madenge amekiri kuwa nyota njema sasa inaonekana kwani ni mwanzo mzuri kuanza kwa zoezi la utwaaji viwanda hasa katika mkoa wake wa Lindi kwani bila hivyo Serikali itakua haiwatendei haki wakulima na wananchi wake kwa ujumla kama viwanda vilivyo karibu nao havifanyi kazi ili kupata soko la malighafi zao ambazo ni mazao yao.

Aidha, Katibu Tawala ameisihi pia Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina kuhakikisha inawafanyia upekuzi wa kina sana kabla ya kuwachagua wawekezaji wanaojitokeza na kuonyesha nia ya kutaka kupatiwa viwanda kwa kubinafsishwa au kuuziwa ili kufanya uwekezaji wenye tija ili kuleta faida itakayochagiza ukuaji wa uchumi wa nchi, kuboresha kipato na hali ya maisha ya mwananchi mmoja mmoja hali kadhalika kukua kwa pato la Taifa.

Taarifa hai ya ufuatiliaji na tathmini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina imeeleza kuwa, “Kulingana na Kifungu 7.1 na 7.2 cha Mkataba, mwekezaji alitakiwa kuwekeza kiasi cha USD 600 kwa ajili ya kufanya ukarabati na kuboresha kiwanda ndani ya miezi sita baada ya kukabidhiwa kiwanda tarehe 11 Mei, 2005; kulingana na kifungu cha Mkataba 5.1. Mwekezaji alifanya uwekezaji mdogo kwa kukarabati baadhi ya mashine pamoja na majengo. 

Hata hivyo, kiwanda kilifanya kazi kwa mwaka mmoja 2007/08 na kusimamisha uzalishaji hivyo mpaka kufikia siku hii ya kutwaliwa hakuna uzalishaji unaoendelea hivyo Serikali imefanya maamuzi ya kukirejesha kiwanda hiki Serikalini kufuatia kusimama kufanya kazi kwa muda mrefu na mwekezaji kutoonesha jitihada zozote za uendelezaji wa kiwanda.”
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )