Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Monday, November 26, 2018

Watatu Washikiliwa Na Jeshi La Polisi Kwa Kukutwa Na Nyara Za Serikali

Na. Vero Ignatus, Manyara
Jeshi la polisi Mkoani Manyara, linawashikilia watu watatu kwa kudaiwa kukutwa na nyara za serikali ikiwemo vipande vitatu vya jino la Tembo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Augostino Senga akizungumza jana alisema watu hao walikamatwa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Top In One iliyopo mtaa wa Oysterbay mjini Babati.

Kamanda Senga aliwataja watu hao kuwa ni Anthony Paschal (28) na Juma Ingi wote wakazi wa Endasak wilayani Hanang' na Tluway Gosi mkazi wa Simbay wilayani Hanang'. Alisema mbinu waliyotumia ni kuficha vipande hivyo ndani ya mfuko wa sulphate kisha kuweka chini ya uvungu wa kitanda ili wakaiuze.

Alisema baada ya timu ya makachero kwa kushirikiana na maofisa wanyamapori wa shirika la hifadhi ya Taifa ya Tarangire kupata taarifa walifika eneo hilo na kuwakamata watu hao. "Watuhumiwa hao wote wanashikiliwa na polisi na tunaendelea na upelelezi kabla ya kuwafikisha mahakama kwa ajili ya kujibu mashtaka yanayowakabili," alisema kamanda Senga.

Katika tukio lingine, kamanda Senga alisema watu watatu wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na lita 40 za pombe haramu ya moshi maarufu kama gongo. Alisema watu walikamatwa juzi kwenye kijiji cha Kazamoyo kata ya Kisangaji wilayani Babati wakiwa wamebeba kwenye pikipiki aina ya Skygo yenye namba za usajili MC 970. Aliwataja watu hao kuwa ni Daniel Hewasi (47) mkazi wa Magugu, Hussein Athuman (50) mkazi wa kijiji cha Kazaroho na Idd Hamis (35) mkazi wa kijiji cha Magugu.

Alisema watu hao walikuwa wamebeba pombe hiyo haramu kwenye pikipiki hiyo wakiwa wamehifadhi kwenye madumu mawili ya lita 20 kila moja.Alisema pikipiki hiyo iliyokuwa imebeba pombe hiyo haramu ni mali ya Idd Hamis na lengo lao ilikuwa ni kwenda kuuza ili kujipatia kipato.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kabla ya kuwafikisha mahakamani wakajibu mashtaka yanaoyowakabili.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )