Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Sunday, November 25, 2018

Waziri Wa Kilimo Atangaza Kiama Kwa Wasambazaji Wa Mbegu Feki

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga, 24 Novemba 2018 ametangaza kiama kwa wafanyabiashara wa mbegu nchini wanaouza Mbegu feki zilizopigwa marufuku na serikali.

Amewataka wafanyabiashara wote wa mbegu ambao wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa kuwauzia wakulima mbegu feki zilizopigwa marufuku na serikali kuacha haraka iwezekanavyo kwani serikali itawachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo ya serikali.

Ametoa agizo hilo akiwa ziarani Mkoani Morogoro ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Taasisi iliyopewa jukumu na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la usajili wa wafanyabiashara wa mbegu (Seed Dealers). 

“Serikali imepokea malalamiko mengi kwa wananchi kuhusu Ubovu wa mbegu jambo ambalo limepelekea kwa kiasi kikubwa kuwa na mavuno kidogo pasina kukidhi matakwa ya wakulima wetu nchini” Alikaririwa Mhe Hasunga

Waziri huyo pia ameiagiza Taasisi ya udhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kutimiza majukumu yao kwa kuwabaini wafanyabiashara wanaokiuka maagizo ya serikali pamoja na taratibu na sheria za nchi. 

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu mbegu feki jambo hili serikali haiwezi kukubaliana nalo hivyo TOSCI wanapaswa kusimamia kwa weledi ukaguzi na usajili wa Mbegu bora, pia ni lazima kuwabaini wasambazaji feki wa mbegu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao” Alisisitiza Mhe Hasunga

Alisema Wizara ya Kilimo imepewa jukumu mahususi la kuhakikisha sekta ya kilimo inaimarika kwa usimamizi madhubuti wa sera, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali hivyo kunapokuwa na kelele za wananchi kuhusu mbegu feki ni dhahiri kuwa Taasisi zenye jukumu hilo hazitekelezi kazi yake kwa weledi.

Mhe Hasunga alieleza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha kuwa inaongeza thamani ya mazao yote yanayozalishwa nchini, sambamba na kutafuta masoko mazuri. 

Vilevile, ameitaja Wizara ya Kilimo kuwa ina wataalamu wengi hivyo unaandaliwa mfumo mzuri wa kuwaunganisha watalaamu hao ili kujadili kwa pamoja namna ambavyo kilimo kinaweza kubadilika kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara ili kutoa malighafi za kutosha zitakazohuisha serikali ya viwanda.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )