Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Saturday, November 17, 2018

Waziri wa Kilimo Awataka Watendaji Kusimamia Ubora Wa Korosho

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara
Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametaka watendaji wa Bodi ya Korosho na Waendesha maghala kusimamia kwa weledi ubora wa korosho ili fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya kununua korosho za wakulima katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zitumike ipasavyo.

Waziri Hasunga ameyasema hayo tarehe 16 Novemba 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

Alisema kuwa baada ya wananchi katika maeneo mbalimbali kusikia kuwa serikali imeanza kuwalipa wakulima wa korosho yamejitokeza matukio ya kuwepo kwa korosho chafu zilizotunzwa kwenye maghala tangu msimu wa mwaka jana 2016/2017 zikiwa hazipo katika ubora unaotakiwa wa daraja la kwanza ilihali korosho za madaraja mengine hazijaanza kununuliwa.

“Nadhani wanafanya hivi ili wafaidike na hela za serikali, jambo hili hatuwezi kukubaliana nalo kwani tayari tumeshakamata Tani 20 za korosho chafu kutoka kwenye ghala la Olam za Chama cha Ushirika cha Mnyawi Amcos kilichopo Nanyamba pamoja na Mbembaleo Amcos ambapo gunia tano za korosho chafu zimepatikana” Alisema

Aidha, Mhe Hasunga alisema kuwa Kuna watu wameanza kuingiza korosho zao kutoka nchi jirani baada ya kusikia kuwa Tanzania inanunua korosho kwa bei nzuri huku akisisitiza kuwa watanzania wanapaswa kushirkiana na vyombo vya dola kutoa taarifa za wahalifu wanaoingiza korosho kinyume na sheria.

Alisema, kuruhusu korosho za nje ya nchi zitaharibu soko ikiwa ni pamoja na kuhatarisha amani ya wananchi waliyonayo katika maeneo yote yanayolima korosho.
“Tutailinda mipaka yetu na kuilinda korosho yetu ambayo tunayo” Alisisitiza Mhe Hasunga

Kuhusu kuanza malipo kwa wakulima Mhe Hasunga alisema kuwa tayari vyama 35 vimekwisha hakikiwa na serikali imeanza kulipa fedha zinazostahili.

Serikali imeshanunua Tani 738.7 huku wakulima wakinufaika na fedha zao ambapo taratibu zingine zinaendelea kwa ajili ya kuhakiki na kukamilisha malipo kwa wakati katika vyama vingine.

“Vyama vilivyohakikiwa ni 35 lakini mpaka sasa kati ya hivyo vyama 6 vimeshaingiziwa fedha ambavyo ni Mtama Amsos, Kitomiki Amcos, Mnazimoja Amcos, Mtetesi Amcos, Chamana Amcos na Msafichema Amcos”

Waziri Hasunga aliongeza kuwa mpaka kufikia jana jioni (Tarehe 16 Novemba 2018) tayari wanachama 2348 walikuwa wamelipwa kupitia njia ya benki huku akisisitiza kuwa serikali ilianza kwanza na mkulima ambapo hatua itakayofuata itakuwa ni kuwalipa wachuuzi sambamba na walinda ghala.

Wakulima wanaendelea kulipwa fedha zao ambapo kilo moja ya koroshwa inanunuliwa kwa shilingi 3300 fedha ambayo inaenda moja kwa moja kwa mkulima bila kukatwa kiasi chochote cha fedha.

MWISHO
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

taboola apo chini
....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )