Sunday, November 4, 2018

Waziri wa Kilimo Dkt Tizeba Awapongeza Wakuu Wa Mikoa Kwa Usimamizi Bora Uliopelekea Kuongezeka Kwa Uzalishaji Wa Pamba

Na Mathias Canal-WK, Mwanza
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) amewapongeza wakuu wa mikoa yote nchini inayozalisha pamba, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kwa usimamizi bora uliopelekea uzalishaji wa zao hilo kuwa maradufu katika msimu wa ununuzi wa mwaka 2018/2019.

Dkt Tizeba ametoa pongezi hizo leo jumapili tarehe 4 Novemba 2018wakati akifungua mkutano wa 14 wa wadau wa sekta ndogo ya Pamba katika mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Benki Kuu Jijini Mwanza na kusema kuwa Uzalishaji wa pamba katika msimu wa ununuzi wa mwaka 2018/19 umeongezeka kwa asilimia 67 kutoka tani 133,000 hadi tani 221,600.

Pamoja na pongezi hizo waziri huyo amewataka viongozi hao kuongeza ufanisi wa usimamizi wa zao hilo kwani pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji lakini bado matarajio ya uzalishaji hayakufikiwa kwa mujibu wa makubaliano.

Alizitaja sababu zilizopunguza uzalishaji kuwa ni pamoja na Ukame mkali kati ya mwezi Januari na Februari ulipukutisha vitumba vichanga; Mripuko wa wadudu wakiwemo viwavi jeshi vamizi, vidung’ata, chawa jani, vithiripi, vidukari. Wadudu wanaofyonza miaka ya nyuma halikuwa tatizo kwenye pamba; Mvua kubwa kupita kiasi kati ya Machi na Mei ilizamisha pamba kwenye maeneo yote ya mbuga na mabondeni; sambamba na Ufahamu mdogo wa wakulima kuhusu matumizi ya viuadudu.

Alisema,  mfumo wa kuzalisha mbegu bora za pamba umefufuliwa na unafanya kazi. Mbegu mama (Breeder seed) inazalishwa katika Taasisi ya Utafiti ya Ukiriguru na inakwenda kupandwa katika shamba la Nkanziga lililopo Wilayani Misungwi ili kuzalisha (Prebasic seed)

Mbegu hiyo inakwenda kupandwa katika Kata ya Mwabusalu wilayani Meatu ili kuzalisha mbegu ya Msingi (Basic seed). Mbegu ikitoka Mwabusalu inakwenda kupandwa Wilaya ya Igunga ili kuzalisha mbegu iliyothibitishwa (Certified Seed).

“Katika kipindi cha miaka 2 tumefanikiwa kuzalisha mbegu mpya ya UKM08 kwa ajili ya wakulima wote wa pamba. Kuanzia msimu huu wa kilimo wa 2018/19 wakulima wote watapanda mbegu mpya ya UKM08. Nichukue fursa hii kuwapongeza Wadau wote mlioshiriki kufanikisha uzalishaji wa mbegu bora kwa ajili ya wakulima wetu” Alikaririwa Dkt Tizeba

Aidha, alisema kuwa Kilimo cha pamba bado kina matatizo ya msingi ikiwemo huduma za ugani kutowafikia wakulima. “Hili ni tatizo kubwa la uendelevu wa kilimo nchini si pamba peke yake. Maelekezo mengi yametolewa kuhusu umuhimu wa kuboresha utoaji wa huduma za ugani, lakini utekelezaji wake ni hafifu. Nakitaka kikao hiki tulijadili suala hili na tuliwekee azimio linalotekelezeka ili tija katika kilimo cha pamba na mazao mengine iweze kuongezeka” Alisema

Pia ameiagiza Bodi ya Pamba kugawa kamba za kupandia kabla ya tarehe 10 Novemba 2018.

Alisema, Uamuzi wa Serikali kubadili mfumo wa ununuzi wa pamba ulipokelewa kwa hisia mbalimbali lakini Vyama vya Ushirika vya Msingi vimesimamia kwa weledi na ufanisi mkubwa zoezi la ununuzi wa pamba.

“Natambua yapo mapungufu yaliyojitokeza katika shughuli ya ununuzi wa pamba ikiwemo AMCOS kupoteza fedha za makampuni ya pamba mfano Wilaya ya Maswa na kuchelewesha kulipa baadhi ya wakulima katika Wilaya za Bunda na Serengeti” 

“Namuagiza Mrajis kuchukua hatua za haraka za kisheria kwa viongozi wote wa AMCOS waliofanya ubadhirifu ili haki itendeke na ionekane inatendeka. Taarifa ya hatua zilizochukuliwa niipate tarehe 30 Novemba 2018” Alisisitiza Dkt Tizeba
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )