Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Monday, November 26, 2018

Wito Watolewa Kwa Kanisa Kuwekeza Kwenye Miradi

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameliomba Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo na huduma mbalimbali za jamii mkoani hapa.

Mtaka ameyasema hayo Novemba 25, wakati alipozungumza na waumini wa Kanisa hilo katika Usharika wa Tumain Bariadi Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, ambapo alikuwa mgeni rasmi katika harambee ya ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa na matundu 10'ya vyoo katika Shule Awali na Msingi ya Tumaini (Tumaini Pre & Primary School) inayomilikiwa na kanisa hilo.

Amesema kanisa hilo limekuwa na mchango mkubwa katika miradi mingi ya maendeleo hususani katika sekta ya elimu, afya, maji na maeneo mengine muhimu ikiwemo sekta ya fedha ambapo Kanisa hilo linamiliki Benki ya Maendeleo.

"Pamoja na mradi huu wa shule ya msingi, tunaendelea kuliomba Kanisa kuona umuhimu wa kuwekeza katika miradi mingine ya maendeleo kwenye mkoa wetu; Kanisa lina hospitali, benki na vyuo vikuu; huu ni mkoa ambao bado haujawa na vyuo vikuu vingi kwa hiyo ipo nafasi kwa kanisa kuona kama linaweza kuwa na chuo cha ufundi, chuo cha kati au Tawi la Chuo Kikuu au kuwekeza katika eneo jingine ."alisema Mtaka.

Aidha, amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kwa kuwa limekuwa sehemu ya mafanikio ya nchi yetu tangu imepata uhuru, kwani wapo Viongozi na Watanzania wengi katika maeneo tofauti nchini ambao wamepata elimu katika Vyuo na shule za kanisa, huku akisisitiza kanisa kuendelea kuombea amani na mshikamo wa nchi.

Naye Askofu wa KKKT, Dayosis ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Dkt. Emmanuel Makala amesema Kanisa litaendelea kushirikiana Serikali katika kuwafanya watu.wamjue Mungu na kuwaletea wananchi maendeleo, ambapo amebainisha kuwa ujenzi wa shule ni moja ya njia za kushirikiana na Serikali katika kuondoa ujinga na kujenga Taifa lenye watu walioelimika jambo ambalo litairahisisha Serikali katika kuwaongoza wananchi wake.

"Kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha watu wa Simiyu katika wilaya zote wanamjua Mungu; tunajenga shule ili tuondoe ujinga watu waelimike, ujinga ukiondoka hata Serikali inapata nafuu kuwaongoza watu wake" alisema Askofu Makala.

Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi, Katibu wa Kamati ya Ujenzi, Mwl. Oberlin Kileo amesema ujenzi wa Shule ya Tumaini ulianza mwaka 2012, ambapo jumla ya vyumba vya madarasa tisa, matundu ya vyoo 10, jiko, stoo na viwanja vya michezo vilijengwa na kugharimu shilingi milioni 200 zikijumuisha na gharama za uwekaji wa miundombinu ya maji na umeme.

Ameongeza kuwa ili kujenga vyumba vya madarasa vitano na matundu 10 ya vyoo vivyokusudiwa kujengwa kwa awamu ya pili jumla ya shilingi milioni 120 zinahitajika.

Katika harambee hiyo jumla ya shilingi 41,526,500/= zilipatikana, kati ya hizo fedha taslimu zikiwa ni shilingi 7,466, 500  na ahadi shilingi 34, 060,000/= pamoja na vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwemo  mifuko 60 ya saruji, nondo tani moja, mchanga lori kubwa nne na kokoto tripu mbili.

MWISHO
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )