Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Tuesday, December 4, 2018

SUMA JKT Yaagizwa Kukabidhi Jengo La Wizara Ya Mifugo Na Uvuvi Desemba 30

Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amemtaka mkandarasi SUMA JKT, aliyepewa kazi ya kujenga jengo la ofisi ya wizara hiyo katika mji wa serikali eneo la Ihumwa, Jijini Dodoma, kuhakikisha jengo hilo linakamilika kwa wakati ifikapo Desema 30 mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kufika katika eneo hilo, kukagua hatua za awali za ujenzi wa jengo la ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, akiambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulika Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatama, Mhe. Ulega alisema zaidi ya Shilingi Bilioni Moja tayari zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo.

“Sisi tunamuahidi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, wizara yetu imeanza kazi ya kujenga jengo letu hapa Jijini Dodoma kwa kufuata maelekezo yake, hivyo tunatarajia kufika Desema 30 mwaka huu tukabidhiwe jengo hili na tuanze kulitumia mara moja, hivyo mkandarasi SUMA JKT ahakikishe anakamilisha jengo kwa wakati, tunajivunia tunahamia rasmi Dodoma kwa vitendo.” Alisema Mhe. Ulega.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, alimweleza Mhe. Naibu Waziri Ulega kuwa jengo hilo linalojengwa kwa sasa ni la awali ambalo litaweza kuwahudumia waziri, naibu waziri, makatibu wakuu pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa wizara hiyo, kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo kubwa katika eno hilo la Ihumwa.

“Mhe. Naibu waziri hili eneo lina ukubwa wa Hekari Sita na sasa katika hatua za ujenzi tunahakikisha, huduma zote muhimu ziweze kufikishwa hapa tukianza kutumia jengo hili ikiwemo huduma ya maji na umeme na pia tunazingatia utunzaji wa mazingira katika ujenzi huu ili eneo hili la mji wa serikali liwe la kipekee hususan katika majengo yetu ya wizara ya mifugo na uvuvi yatakayojengwa.” Alisema Prof. Gabriel 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatama alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inatarajia kuanza mchakato wa kujenga jengo kubwa katika eneo hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuwahudumia wafanyakazi wote wizara hiyo waliopo makao makuu ya nchi Mjini Dodoma.

“Tunajitahidi kuhakikisha tunakamilisha dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt John Magufuli, kuhakikisha tunakuwa na jengo letu na katika bajeti ijayo tunatarajia kutenga fedha ambazo zitawezesha kujenga jengo kubwa, kwa sasa tunajenga hili ambalo litatumika na viongozi kutii agizo la mheshimiwa rais.” Alisema Dkt. Tamatama.

Eneo la Ihumwa katika Mji wa Dodoma ni eneo rasmi ambalo limetengwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya serikali yakiwemo ya wizara ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ofisi za serikali kuhamia rasmi Mjini Dodoma, kutokana na agizo lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakati akiingia madarakani mwezi Novemba mwaka 2015, ambapo kwa sasa ofisi mbalimbali za serikali zinafanya shughuli zake katika majengo ya kupangisha.

MWISHO.

Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
                   Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )