Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Thursday, January 17, 2019

Naibu Waziri Dk Mabula Atoa Onyo Kali Kwa Watendaji Wa Sekta Ya Ardhi Pwani

Na Munir Shemweta, KIBAHA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula ametoa  onyo kali kwa Wakuu wa Idara za ardhi watatu pamoja na Afisa ardhi Mteule mmoja katika halmashauri za Mji na wilaya za Kibaha na Bagamoyo mkoa wa Pwani kutokana na kushindwa kusimamia vizuri majukumu yao.

Dk Mabula amewapa miezi miwili kuanzia tarehe 16 Februari hadi 31 Marchi,2019 watendaji hao wawe wametekeleza maagizo waliyopewa ya kuingiza viwanja na mashamba kwenye mfumo  wa  malipo ya kodi ya ardhi kwa njia ya kielektronik pamoja na kutoa hati za madai kwa wadaiwa wote sugu na wasipotekeleza maagizo hayo ndani ya muda huo watawajibishwa.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa onyo hilo jana wakati alipofanya ziara ya kushtukiza ktika halmashauri za wilaya za Bagamoyo, Chalinze na Kibaha mkoa wa Pwani kuangalia utekelezaji wa maelekezo aliyoatoa kuhusiana na ukusanyaji kodi ya ardhi, uingizaji wamiliki wa viwanja katika mfumo wa kielektronik, utoaji hati za madai kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi pamoja na kushughulikia migogoro ya ardhi.

Watendaji waliopewa onyo kali ni Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha Lucy Kimoi, Mjaliwa Jafari Mwamba Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini,, Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Khalid Tumbulegen pamoja na Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Gilly Simiyu .

Dk Mabula ameshangazwa na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri hizo kushindwa kusimamia sekta hiyo vizuri pamoja na kuwepo mfumo rahisi wa kufuatilia wamiliki wa viwanja na mashamba jambo alilolieleza kuwa linaloikosesha serikali mapato mengi yatokanayo na kodi ya ardhi,

Alisema, pamoja na baadhi ya halmashauri kuonekana kuvuka zaidi ya asilimia hamsini ya makusanyo ya kodi ya ardhi kufikia mwezi Desemba 2018 lakini bado nyingi ya halmashauri hizo zina wadaiwa wengi wenye kiasi kikubwa cha fedha ambapo kama kingekusanywa basi serikali ingeweza kupata fedha nyingi kupitia sekta hiyo.

Dk Mabula ameshangazwa na halmashauri ya Mji wa Kibaha kushindwa kusimamia vyema utoaji hati za madai kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi ambapo kwa mujibu wa Mkuu wake wa idara Lucy Kimoi halmashauri hiyo ilipeleka hati za madai kwa wadaiwa kumi tu wakati ina wadaiwa zaidi ya mia mia mbili jambo lililomfanya Naibu Waziri Mabula kuhoji ni vigezo gani vilitumika kupeleka hati za madai kwa wamiliki kumi tu huku wengine wakiachwa.

Aidha, upande wa halmashauri ya Kibaha Vijijini Kaimu Mkuu wa Idara Jafari Mwamba alimueleza Dk Mabula kuwa halmashauri hiyo haikutoa hati hata moja za madai kwa kuwa viwanja vingi katika maeneo hayo ni vipya na ni vigumu kuwapata baadhi ya wamiliki ili kuwapatia hati za madai jambo lililomuudhi Naibu Waziri ambaye aliwataja baadhi ya wamiliki wa mashamba wanaodaiwa kodi ya ardhi kulingana na kumbukumbu za Wizara.

‘’Mko serious kweli! mkuu wa idara upo na kuna fedha nyingi ziko nje ni vigezo gani mmetumia kuwapelelekea hati za madai wadaiwa kumi tu huku mkiwaacha wengine ambao wana zaidi ya miaka mine hawajalipa kodi ya ardhi’’ alisema Dk Mabula.

Naibu Waziri Dk Mabula alisema, mji wa Kibaha kwa sasa unakuwa kwa kasi hivyo watendaji wa sekta ya ardhi wanapaswa kuhakikisha wanaingiza katika mfumo viwanja na mashamba kufikia tarehe 31 Machi 2019 sambamba na viwanja vipya vitakavyopimwa na asingependa kuona halmashauri hizo zinashindwa kuviingiza kwa visingizio mbalimbalimbali.

Akigeukia halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo, Dk mabula amekerwa na jinsi idara ya ardhi ilivyokalia Hati za Wamiliki wa viwanja bila ya kuwapatia wenyewe kwa visingizio mbalimbali ikiwemo kutokamilika taratibu za kupatiwa hati huku baadhi ya hati zikiwa katika ofisi hiyo kwa zaidi ya miaka miatatu na kuagiza wamiliki wenye hati zao watafutwe kwa kupigiwa simu ili kama kuna dosari wafahamishwe na kurekebishwa.

Dk Mabula amemuagiza Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri hiyo ya wilaya ya Bagamoyo Khalid Tumbulegen kuhakikisha anakamilisha hati hizo ndani ya miezi miwili na kuwapatia wamiliki wake hati zao vinginevyo atakumbana na rungu la kuondolewa katika nafasi hiyo.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Mabula katika kipindi kifupi cha wiki mbili amefanya ziara ya kushtukiza katika halmashauri mbalimbali nchini lengo likiwa kuangalia namna halmashauri hizo zinavyotekeleza maelekezo yaliyotolewa na Wizara kwa lengo la kuongeza ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi na hadi sasa ametembelea baadhi ya halmashauri kwenye mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita, Tanga na Pwani. 
tangazo
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )