Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Friday, January 25, 2019

Serikali Yatoa Bilioni 2.5 Kwa Ajili Ya Ujenzi Wa Jengo La Mama Na Mtoto Hospitali Ya Rufaa Ya Mkoa Wa Shinyanga

NA WAMJW-SHINYANGA
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa kiasi cha shilingi bilioni 2.5 zitakazotumika katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, lengo likiwa ni kutoa huduma za kibingwa kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea ujenzi wa Hospitali hiyo na kukuta jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na Utawala likiwa limekamilika.

Waziri Ummy amesema fedha hizo zitafika katika Hospitali hiyo ndani ya wiki mbili ili ziweze kuchochea kasi ya ujenzi na lengo ifikapo mwezi Septemba 2019 Hospitali hiyo ianze kutoa huduma za afya.

“Ninaahidi kutoa shilingi bilioni 2.5 ndani ya wiki mbili ziweze kutumika katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto, lengo la serikali ni kuhakikisha kila mama mjamzito anapofika Hospitalini kujifungua atoke akiwa salama yeye na kichanga chake”. Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amefikia uamuzi huo baada ya kupokea ripoti ya mkoa kuhusu vifo vitokanavyo na uzazi kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Mfaume Rashid, ambapo kwa mwaka 2016/2017 kulikua na vifo 73, na mwaka 2017/2018 vikiwa ni vifo 56, hali ambayo Waziri huyo ameonekana kutoridhishwa nayo.

Hata hivyo Waziri Ummy ameahidi kuongeza fedha zingine kiasi cha shilingi bilioni 3 ndani ya mwezi mmoja, zitakazotumika katika ujenzi wa jengo kwa ajili ya huduma za uchunguzi ikiwemo huduma za maabara, X-ray na CT-Scan pia jengo hilo litakua na vyumba vitatu vya upasuaji.

Waziri Ummy amesisitiza ujenzi wa jengo hilo utumike wa mfumo wa Force Account ambao utahakikisha wananchi wanashiriki kwa asilimia 100 katika kufanikisha ujenzi huo na huduma za afya zianze kutolewa mapema.

Wakati huo huo, Waziri Ummy ametembelea kituo cha afya cha Kambarage katika Manispaa ya Shinyanga kuona hali ya miundombinu ya kituo hicho na utoaji wa huduma za afya huku kwa kiasi kikubwa akionekana kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa majengo ya huduma mbalimbali.

Kuhusu uhaba wa watumishi wa kada za afya Waziri huyo ameahidi kutatua changamoto hiyo hali inayopelekea kuwepo kwa msongamano wa wagonjwa.

Aidha, Waziri Ummy amehitimisha ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na kuridhishwa kwa kiasi kikubwa na hali ya utoaji wa huduma za afya hasa katika jengo la huduma za mama na mtoto na pia katika jengo la kuhifadhia watoto wachanga wenye uhitaji wa uangalizi maalumu (NICU)
tangazo
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )