Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Tuesday, January 1, 2019

Waziri Mkuu Apokea Vyumba Vya Madarasa

adv1
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa  amepokea msaada wa vyumba viwili vya madarasa vikiwa na  madawati vyenye thamani ya sh. milioni 80 kutoka kwa bank ya CRDB.

Alipokea madarasa hayo jana (Jumatatu, Desemba 31, 2018) katika shule ya Sekondari  Kassim Majaliwa iliyopo Kata ya Nachingwea katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi

Waziri Mkuu aliushukuru uongozi wa benki ya CRDB kwa msaada hu ambao umesaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa unaoikabili wilaya hiyo.

Kadhalika, Waziri Mkuu alizitaka taasisi nyingine ziige mfano wa bank ya CRDB kwani imekuwa bega kwa bega na Serikali katika kuchangia shughuli za kimaendeleo nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Kassim Majaliwa kutumia vizuri madarasa hayo na kutunza mali zilizopo shuleni hapo.

Alisema ujenzi wa shule hiyo ni mradi uliobuniwa na wakazi wa kata ya Nachingwea ili kuwawezesha watoto wao kupata elimu katika eneo lililo karibu na makazi yao.

Waziri Mkuu alisema awali wanafunzi wa kata hiyo walikuwa wanatembea umbali mrefu hadi shule ya sekondari ya Ruangwa jambo ambalo lilikuwa ni changamoto kwao.

“Nawaomba wananchi wenzangu tuendelee kushirikiana katika kuibua na kubuni miradi mbalimbali kwa ajili ya kuboresha maendeleo kwenye kata yetu ya Nachingwea.”

Pia Waziri Mkuu alikabidhi kompyuta 20 kwa shule za sekondari tano ambazo ni Kassim Majaliwa, Likunja, Mnacho, Hawa Mchopa na Ruangwa.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema benki yao inathamini elimu na imekuwa ikirudisha kwa jamii faida wanayoipata kwa kuchangia shughuli za maendeleo.

Alisema mbali na msaada huo wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na madawati yake, pia aliahidi kutoa sh. milioni 20 ili zitumike kununulia madawati yatakayosaidia kupunguza changamoto ya madawati wilayani Ruangwa.

Kwa upande wao, wakazi wa kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa waliishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono katika mradi wa ujenzi wa shule hiyo ya sekondari ambayo imewawezesha watoto wao kusoma karibu na maeneo yao ya makazi yao.

Mmoja wa wakazi hao Omari Losi alisema ujenzi wa shule hiyo utawarahisishia wanafunzi kwenda shule na kuwaondolea shida ya kutembea umbali mrefu kwenda shule ya sekondari ya Ruangwa walikokuwa wakisoma awali.

Naye, mkazi mwingine wa kata hiyo ya Nachingwea, Mariam Kingamkono alisema uwepo wa shule ya sekondari katika kata yao kumeongeza hamasa ya wanafunzi kupenda kusoma kwa sababu wameondolea shida ya kutembea umbali mrefu.

Alisema shule hiyo inawalimu wazuri na wa kutosha na ina mazingira mazuri ya kujifunzia, hivyo aliwaomba wazazi wenzake waendelee kushirikiana na Serikali katika kuboresha maendeleo kwenye kata yao hususan ujenzi wa shule.


 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )