Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Thursday, February 14, 2019

Sheria Ya Maadili Imezidi Kuimarisha Nidhamu Kwa Viongozi Na Watumishi Wa Umma

Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
UONGOZI bora na utawala wa sheria ni vichocheo muhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia mifumo wa uwazi na uwajibikaji, hatua inayolenga katika kuongeza ubora wa utoaji huduma kwa umma.

Kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, jamii itakuwa na utawala bora na utawala wa sheria kama itakuwa na sifa nne ambazo ni pamoja na jamii yenye maadili mema na kuthamini utamaduni, jamii yenye uadilifu na kuheshimu utawala wa sheria.

Sifa nyingine ni jamii isiyokuwa na rushwa na maovu mengine, iliyoelimika na inayojiamini, inayojifunza kutokana na uzoefu wake na wa wengine, na yenye kumiliki na kubaini ajenda za Maendeleo.

Ili kuwa na sifa hizi Serikali iliweka mikakati mbalimbali yenye kujenga maadili mema kwa kuwa na viongozi waadilifu, wanaofuata maadili ya kazi zao katika kutekeleza majukumu yao.

Aidha, viongozi wa umma wakiwa na dhamira timilifu juu ya uadilifu, ni rahisi kwa wananchi kujifunza na kuiga maadili mema kutoka kwao, kwa vile kauli na matendo yao yanatoa mfano mwema katika kuwaelekeza wananchi kuwa waadilifu pia.

Kwa kutambua umuhimu wa kujenga jamii yenye maadili mema Tanzania, Serikali ilianzisha Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi na Watumishi wa Umma ili kufuatilia maadili na mwenendo wa viongozi wa umma.

Sekretarieti ya Maadili inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya viongozi wa umma, namba 13 ya mwaka 1995, inayowataka viongozi na wanasiasa kutoa tamko rasmi kuhusu mali na madeni yao baada ya uteuzi, kila mwisho wa mwaka na baada ya kuacha wadhifa.

Takwimu za urudishaji fomu za tamko la mali kwa viongozi wa umma na viongozi wa kisiasa zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2010/11 na 2013/14 namba ya viongozi waliojaza na kurejesha fomu za tamko imeongezeka zaidi ya mara mbili; kutoka viongozi 3,770 mpaka viongozi 8,400 kwa mwaka.

Inaelezwa kuwa ongezeko hilo lilitokana na hatua ya Serikali ya mwaka 2011 ya kuanzisha Baraza la Maadili ya Utumishi wa Umma ili kusikiliza malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma kama yanavyowasilishwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika anasema hadi kufikia Machi 2018 jumla ya Viongozi wa Umma 16,050 ambao ni sawa na asilimia 98 wamerejesha fomu za tamko la rasilimali na madeni.

Anaongeza kuwa Sekretarieti kwa kushirikiana na wadau imeanza maandalizi ya mchakato wa ujazaji fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya www.ethicssecretariat.go.tz

Aidha Mkuchika anasema katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018, Sektretarieti ya Maadili imepokea na kuchambua Malalamiko 154 ya ukiukwaji wa maadili dhidi ya Viongozi wa Umma, ambapo , malalamiko 119 yalihusu Sheria ya Maadili ya Viongozi na malalamiko 35 hayakuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kwa mujibu wa Mkuchika anasema na malalamiko 35 ambayo hayakuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma walalamikaji walipewa ushauri na mengine yalielekezwa kwenye mamlaka zinazohusika.

Akifafanua zaidi Mkuchika anasema katika mwaka 2017/18, Serikali kupitia Sekretarieti ya Maadili ilianza zoezi la uchambuzi wa nyaraka za uthibitisho wa tamko linalotolewa na Viongozi wa Umma  linahusu ufuatiliaji wa mienendo ya kimaadili yao, ambapo awamu ya kwanza ya uhakiki wa viongozi 1,000 ilikamilika mwezi Aprili, 2018.

Anaongeza kuwa katika kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa Ofisi hiyo, jumla ya watumishi  Watumishi 30 wa Sekretarieti wa kada mbalimbali wamejengewa uwezo katika eneo la utunzaji wa siri, masijala na uhifadhi wa kumbukumbu na nyaraka za ofisi.

Anasema rasimu ya kanuni za Maadili kwa ajili ya utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeandaliwa na maoni ya wadau mbalimbali yanaendelea kupokelewa ili kuboresha kanuni husika.

Uongozi bora na utawala wa sheria ni vichocheo muhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia mifumo ya uwazi na uwajibikaji hatua inayolenga kuhamasisha ubunifu, ustadi, uvumbuzi na kuongeza ubora katika utoaji wa huduma kwa umma.

Aidha, viongozi wa umma wakiwa na dhamira timilifu juu ya uadilifu, ni rahisi kwa wananchi kujifunza na kuiga maadili mema kutoka kwao, kwa vile kauli na matendo yao yanatoa mfano mwema katika kuwaelekeza wananchi.
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )