Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Monday, February 18, 2019

Waziri Biteko Aiagiza Tume Ya Madini Kuziandikia Hati Ya Makosa Leseni Za Madini 18,341

adv1
Greyson Mwase, Asteria Muhozya na Nuru Mwasapeta
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameiagiza Tume ya Madini  kuziandikia hati za makosa leseni za madini 18, 341 zinazodaiwa ili zilipe madeni hayo ndani ya siku 30 na wakishindwa kulipa madeni hayo ndani ya muda huo, leseni hizo zifutwe ndani ya siku saba baada ya mwisho wa hati za makosa.

Waziri Biteko ametoa agizo hilo jijini Dodoma leo tarehe 18 Februari, 2019 kupitia mkutano wake na waandishi wa habari ambao umewashirikisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Kamishna kutoka Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Amesema kuwa zoezi husika lifanywe kwa mujibu wa kifungu cha 63 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 na kusisitiza lisiangalie nani anamiliki leseni hiyo hata kama ni taasisi ya Serikali.

“ Hata ile leseni ya Liganga na Mchuchuma ambayo inamilikiwa na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na mbia wake najua inadaiwa ada ya Dola za Marekani zaidi ya 375,000, sheria ifuate mkondo wake,” alisema Biteko

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko aliiagiza Tume ya Madini kufuta leseni zote za utafiti ambazo zipo hai na hazina madeni, lakini toka zitolewe imepita miezi mitatu bila kuanza kuandaa na kukusanya vifaa stahiki  kwa ajili ya utafiti au imepita zaidi ya miezi zaidi ya sita bila kuanza kufanya utafiti kwani ni kinyume na kifungu cha 36(1) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017.

Aidha aliiagiza Tume ya Madini kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyoainishwa na kutangazwa na Serikali  kwa ajili ya wachimbaji wadogo yatolewe leseni za uchimbaji mdogo tu kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 na yasitolewe kwa uchimbaji wa kati wala mkubwa ili kuwaendeleza na kuwaimarisha kiuchumi wachimbaji wadogo

Alisema kuwa, kuna baadhi ya maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo likiwemo eneo la Melela lilipo mkoni Morogoro ambapo yalitolewa leseni bila kufuata taratibu za utoaji leseni katika maeneo hayo kama zilivyoainishwa kwenye kanuni ya 17 (3) ya Kanuni za Madini, 2018 na kumwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kuwasimamisha kazi pamoja na kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wote waliohusika kwenye utoaji wa leseni hizo.

Pia, aliongeza kuwa katika uchenjuaji wa madini kumekuwepo na tabia ya wachimbaji wadogo wa madini kujenga mitambo ya kuchenjua dhahabu  bila kufuata taratibu ambapo hadi kufikia Februari, 2019 mitambo takribani 639 haina leseni, hivyo kuisababishia Serikali kukosa jumla ya  shilingi bilioni 1.76, zitokanazo na ada ya maombi na ada ya mwaka ya mitambo hiyo.

Aliiagiza Tume ya Madini kuhakikisha kuwa mitambo yote ya uchenjuaji inapatiwa leseni ndani ya siku 30 na kusisitiza kuwa mitambo ambayo itakuwa haijapata leseni ndani ya muda ulioelekezwa haitaruhusiwa kuendelea kufanya kazi na wahusika wote watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aliwataka wenye mitambo husika kufika katika ofisi za mikoa na kuweka mambo sawa na kuongeza kuwa iwapi watakuta vikwazo vyovyote kwenye ofisi za mikoa wawapigie simu kama viongozi na vikwazo vyao kushughulikiwa mara moja.

Aliiagiza Tume ya Madini kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa wote nchini kutenga eneo moja kwa kila mkoa na kusimamia ujenzi wa mitambo ya uchenjuaji madini lengo likiwa ni kuimarisha usimamizi na makusanyo ya mapato katika mitambo hiyo na kusisitiza kuwa zoezi likamilike ndani ya miezi mitatu.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko aliagiza Wizara kuwasimamisha kazi watendaji waliohusika katika utoaji wa leseni ndogo za uchimbaji wa madini kwa wageni jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 kinachokataza leseni ndogo ya uchimbaji wa madini kutolewa kwa wageni.

Mbali na Biteko kuitaka Tume ya Madini kufuta leseni za uchimbaji mdogo wa madini  zilizotolewa kwa wageni aliitaka Tume ya Madini kutokutoa leseni mpya kwa kampuni au mtu binafsi aliyepewa hati ya makossa na kushindwa kurekebisha marekebisho hayo kwa kuwa ni kinyume na Kifungu cha 31(b) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017.

Aidha, aliwataka wachimbaji wadogo nchini kutafuta njia mbadala ya kuzuia mashimo yao kuanguka kwa kutumia zege na vyuma badala ya kutumia miti lengo likiwa ni kutunza mazingira kwa vizazi vijavyo na kusisitiza kuwa baada ya mwaka mmoja Serikali haitaruhusu tena magogo kutumika kwenye mashimo ya uchimbaji wa madini .

Awali akielezea mafanikio ya Wizara ya Madini, Biteko alisema kuwa katika bajeti ya   mwaka wa fedha wa 2018/2019, Wizara pamoja na mambo mengine iliahidi kuendeleza uimarishaji  wa uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na uendeshaji wa biashara katika sekta ya madini.

Alisema Wizara iliratibu mafunzo kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchi nzima kwa kipindi cha mwezi Januari, 2019 ambapo yalifanyika kikanda katika vituo vya Singida, Chunya, Mpanda, Handeni, Buhemba, Kelwa na Bukombe ambapo yalilenga kuwapa wachimbaji wadogo taarifa sahihi za aina na kiasi cha mashapo ya madini yanayopatikana katika maeneo yao na aina ya teknolojia inayoweza kutumika katika uchenjuaji wa madini hayo.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya umahiri na vito vya mfano ambapo uligharimu shilingi bilioni 12 na kusisitiza kuwa vituo vinatarajiwa kuzinduliwa mwezi Machi, 2019 mara baada ya ujenzi wake kukamilika.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwezi Januari, 2019 Wizara ilifanya uhakiki wa leseni zote za uchimbaji wa madini ambazo zimetolewa na kubaini leseni nyingi hazijafuata matakwa ya kisheria ambayo ni pamoja na  kuhodhi au kushindwa kuendeleza maeneo ya utafiti waliyopewa kinyume na kifungu cha 36 (1) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 ambapo imepelekea kukosesha wachimbaji wengine haswa wadogo maeneo ya kuchimba na kusababisha malalamiko kwa Serikali.

Alitaja matakwa mengine yaliyokiukwa kuwa ni pamoja na kushindwa kulipa malipo stahiki ya Serikali ikiwa ni pamoja na Ada ya Mwaka kinyume na kifungu cha 92 (1) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017,ambapo kama fedha hizi kama zingepatikana zingeisaidia Serikali kutoa huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na afya, elimu, maji na miundombinu.

Alisema uhakiki wa leseni za madini ulionesha kuwa, hadi kufikia Februari, 2019 jumla ya leseni 18,341 kati ya leseni 30,973 ambazo zipo hai zinadaiwa jumla ya shilingi bilioni 116.67 ambapo leseni kubwa za utafiti zinadaiwa shilingi bilioni 61.67, leseni za uchimbaji mkubwa zinadaiwa shilingi bilioni 6.41, leseni za uchimbaji wa kati zinadaiwa shilingi bilioni 28.28 na leseni za uchimbaji mdogo wa madini zinadaiwa shilingi bilioni 19.51.
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )