Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Wednesday, March 6, 2019

Serikali Yajitosa Kutatua Mgogoro Wa Wawekezaji Wa Kilimo Cha Kahawa Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro

adv1
Na Josephine Majura na Peter Haule, WFM, Kilimanjaro
Serikali  imeitaka Kampuni ya Tudeley Estates Limited  kutoka Uingereza  iliyoingia mkataba na vyama vya Ushirika Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro vinavyojishughulisha na uwekezaji wa Kilimo cha Kahawa (Murososangi), kurudi nchini ili kufanikisha utatuzi wa mgogoro uliosababishwa na kuibuka kwa mwekezaji mpya ambae mkataba wake haujulikani.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angela Kairuki walipofanya mkutano na Wawekezaji, Vyama vya Ushirika na Wadau wengine kuhusu mgogoro na Mwekezaji huyo Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Dkt. Mpango alisema kuwa, Vyama vya Ushirika vya Murososangi, viliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited ya nchini Uingereza ambapo washirika hao wenye mashamba eneo la Kibo na Kikafu  wilayani Hai, yenye ukubwa wa hekari 2054 walimpa Mwekezaji huyo ili kuendeleza zao la kahawa kuanzia mwaka 1998.

Alisema kuwa baada ya mwekezaji  huyo, Bw. Conrad Legg, kuonesha nia ya kutoendelea na uwekezaji huo aliondoka nchini, wakaja wawekezaji wengine kutoka Ujerumani ambao waliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited, kwa kununua hisa bila  kuvishirikisha Vyama vya Ushirika vilivyoingia mkataba wa awali jambo lililosababisha sintofahamu kwa wana ushirika hao.

“Aliyeingia mkataba na Murososange, arudi nchini ili kutatua mgogoro huo ili kuona Wananchi wanawezaje kuingia mkataba mwingine na mwekezaji mpya ambao utalinda maslahi ya wananchi wenye mashamba hayo na pia mwekezaji”, alisema Dkt. Mpango.

Alisema Wanaushirika hao wanataka Mwekezaji wa kwanza arudi nchini ili wavunje mkataba wa awali kwa kuwa mkataba huo haujaisha muda wake hivyo hawawezi kuingia mkataba na mwekezaji mpya wakati ule wa awali bado unaendelea.

Aidha, alisema kuwa mwekezaji mpya kutoka Ujerumanim Bw. Marcus Shiber,  alianza kuleta fedha katika eneo la uwekezaji  na kulipa baadhi ya kodi za mtangulizi wake, madeni, mishahara na kuboresha miundombinu ya mashamba hayo bila kupata muafaka na Vyama vya Ushirika jambo ambalo liliendelea kuleta mgogoro.

Dkt. Mpango alisema kuwa, wamepata maelezo kutoka pande zote na baadhi ya maelezo hayo yanahitaji ushauri wa kisheria hivyo tumeiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuyafanyia kazi mambo hayo ili kuweza kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, namna bora ya kumaliza mgogoro huo bila kuingizia Serikali hasara.

Aliwatahadharisha watendaji wakuu wa serikali kutotumia ubabe na vitisho kwa wawekezaji ili kutoharibu taswira ya taifa katika masuala ya uwekezaji unaopigiwa chapuo hivi sasa na Serikali ya Awamu ya Tano, ili kuvutia mitaji, mapato ya serikali, ajira kwa vijana na kuvutia teknolojia za kisasa kwa maendeleo ya Taifa.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Angela Kairuki, alisema kuwa kutokana na mgogoro huo wa kiuwekezaji akaunti za Mwekezaji mpya kutoka Ujerumani ikiwemo ya Kampuni ya Kuza Afrika inayojishughulisha na kilimo cha parachichi Mkoani Mbeya ilifungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kuhusiana na masualaya kodi, jambo lililosababisha baadhi ya shughuli za Mwekezaji huyo kukwama.

Alisema kuwa kikosi chao kupitia Waziri wa Fedha na Mipango aliyetumwa na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kutatua mgogoro huo, wameangalia iwapo taratibu za kufungwa akaunti hizo zilifuatwa na kutafuta njia bora ya kutatua tatizo hilo na pia kuona ni Mwekezaji yupi anafaa kuingia mkataba na Vyama vya Ushirika vya Murososangi, nia ikiwa ni kuona Vyama hivyo vinanufaika na Uwekezaji unakua nchini.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mgwira, aliishukuru Serikali kwa hatua yake ya kutuma Mawaziri ili kutatua mgogoro huo wa muda mrefu ambao utatuzi wake utasaidia Wananchi kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini-TIC, Bw. Geofrey Mwambe, alisema kuwa katika mkutano kati ya Mawaziri, Wawekezaji na Vyama vya Ushirika wamebaini kuwa utaratibu walioukuta Wawekezaji kutoka Ujerumani haukuwa sawa na ule ambao waliwekeana na Mwekezaji wa kwanza kutoka Uingereza, hivyo kuleta ugumu kiutendaji kwa Mwekezaji wa pili.

Alisema kuwa, Serikali inahitaji uwekezaji katika Sekta ya Kilimo ili  kupata malighafi ya viwanda nchini, kuongeza mnyororo wa thamani na kukuza pato la Taifa, hivyo inafanya jitihadi za kuvutia wawekezaji watakaoleta mitaji na teknolojia ya kisasa ili Taifa liweze kukabiliana na ushindani wa bidhaa katika soko la Kimataifa.

Mwakilishi wa mwekezaji mpya kutoka Ujerumani Bw. Robert Clowes, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuwatuma Mawaziri wake kuja kutatatua mgogoro huo, alisema Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji hivyo yupo tayari kuendelea kuwekeza zaidi nchini kwa lengo la kupata manufaa kwa pande zote ikiwa ni pamoja na Kampuni yake na vyama vya ushirika wa kilimo cha Kahawa Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Mwisho.
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )