Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Wednesday, March 6, 2019

Waziri Mkuu Atembelea TFDA na TBS....Awataka Mawaziri Watano Wakutane Haraka na Wampe Majibu Ifikapo March 30

adv1
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri wa Kilimo, Uwekezaji, Viwandana Biashara, Mifugo na Uvuvi na Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakutane na wafanye mapitio ya taasisi zao na kuangalia maeneo yanayogongana kiutendaji ili kila mmoja abaki na jukumu lake.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Machi 6, 2019) alipotembelea Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hizo na amewaagiza mawaziri wakutane na wampelekee taarifa ya mapendekezo yao ifikapo Machi 30, 2019.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa malalamiko na manung’uniko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wamedai kuwepo kwa muingiliano wa majukumu ya kiutendaji ya taasisi hizo, hivyo kuwasababisha washindwe kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Waziri Mkuu amesema taasisi hizo zinashughuli ambazo zinaingiliana na kusababisha malalamiko kwa wateja wao, ambapo ametolea mfano suala la kudhibiti ubora wa bidhaa ambalo linafanywa na TFDA na TBS kwa mujibu wa sheria. Amewataka wapitie sheria zao na wajue ukomo majukumu yao.

“Kutaneni pitieni maelekezo ya Serikali yanayoelekeza namna ya kuzifanya taasisi hizi na zingine zinazofanya shughuli zinazofanana zilizo katika wizara zenu bila kusanau Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (blue print). Ifikapo tarehe 30 mwezi huu niwe nimepata mapendekezo yenu,” amesisitiza.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa taasisi hizo wabadilike na waache urasimu kwasababu hauna tija katika utekelezaji wa majukumu yao na badala yake unaweza kuwayumbisha kwenye ufanyaji wao wa kazi. “Kila mmoja atekeleze majukumu yake kwa uzingatia maadili ya taaluma yake.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka waangalie namna ya kuwahisha majibu ya vipimo vya bidhaa wanazoletewa na wateja, kama watakuwa wamekamilisha kabla ya siku za kisheria wawajulishe wateja wao na kuhusu sampuli ambazo zitakuwa hazijaharibika wakati wa vipimo wawarudishie.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi hizo ziangalie namna ya kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuwa na watumishi katika ngazi za wilaya na kwa TFDA ameitaka ianzishe maabara nyingine mbili kwenye kanda ya Nyanda za Juu Kusini na ya Kaskazini ili kusogeza huduma kwa wananchi.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MACHI 6, 2019.
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )